
NYON, USWISS: Leo ndiyo Leo kwenye usiku wa upangaji wa droo ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Baada ya juzi usiku kushuhudiwa miamba mingine nane ikitinga hatua hiyo baada ya michezo ya mtoano na kuungana na nyingine nane zilizofuzu awali katika hatua ya ligi.
Katika hatua hiyo ya mtoano kwa zile zilizomaliza katika nafasi za chini, ilishuhudiwa miamba mikubwa ikiwamo Manchester City na AC milan zikitolewa huku Paris Saint-Germain, Benfica, Feyenoord, PSV Eindhoven, Borussia Dortmund, Club Brugge, Bayern Munich na Real Madrid zikiungana na zilizopita mapema katika ligi.
Timu zilizofuzu moja kwa moja ni Liverpool, Barcelona, Arsenal, Inter Milan, Atletico Madrid, Bayer Leverkusen, Lille na Aston Villa na sasa shauku kubwa ya mashabiki wa soka ni kujua nani atapangwa na nani katika hatua hiyo ambayo droo yake itachezeshwa kuanzia saa 8:00 mchana huko Nyon, Uswizi.
Baada ya mchezo uliokuwa ukifuatiliwa na wengi kushuhudia Madrid ikiichapa Man City jumla ya mabao 6-3, kilichopo ni huenda miamba hiyo ya Santiego Bernabeu ikakutanishwa na majirani zao Atletico Madrid au Bayer Leverkusen inayofundishwa na mchezaji wao wa zamani Xabi Alonso, sawa na Bayern Munich ambayo iliichapa jumla ya mabao 3-2 Celtic na wapinzani wao hao walimaliza kati ya timu nane za awali.
Tayari imeshaonekana timu zipi zinaweza kukutana kwa mujibu wa ratiba ilivyo huku PSG iliyofuzu kibabe inaweza kukutana na ama Liverpool au Barcelona zilizomaliza kati ya timu nane za juu sawa na Bnfica ambayo ilifuzu kwa kuitoa AS Monaco.
Club Brugge iliyoitoa Atalanta kwa jumla ya mabao 5-2 na Borussia Dortmund moja inaweza ikakutana na ama Lille iliyomaliza nafasi ya saba au Aston Villa nafasi ya nane.
Vijana wa Mikel Arteta, Arsenal pamoja na Inter Milan kwenye hatua hii ya 16 bora zitakuwa na safari ya kwenda Uholanzi kwani zinaweza kukutana na timu moja kati ya mbili kutoka nchi hiyo PSV Eindhoven na Feyenoord.
Baada ya hatua ya 16 bora, hakutokuwa na droo ya robo fainali na badala yake timu mshindi wa mchezo wa mtoano kati ya PSG dhidi ya Liverpool au Barcelona itakutana na mshindi kati ya Club Brugge dhidi ya Lille au Aston Villa.
Mshindi wa mchezo kati ya Real Madrid dhidi ya Atletico Madrid au Bayer Leverkusen atakutana na mshindi kati ya PSV dhidi ya Inter Milan au Arsenal.
Vile vile mshindi wa mchezo wa hatua ya 16 bora kati ya Feyenoord dhidi ya Inter Milan au Arsenal atakutana na mshindi wa mchezo Bayern Munich dhidi ya Bayer Leverkusen au Atletico Madrid.
Robo fainali ya mwisho inaweza kuwa kati ya mshindi wa mchezo wa hatua ya 16 bora utakaozikutanisha Dortmund dhidi ya Aston Villa au Lille na mshindi wa mechi ya Benfica dhidi ya Liverpool au Barcelona.
Mechi za mkondo wa kwanza za robo fainali zitapigwa kati ya April 08 na 09 na mkondo wapili ni kati ya April 15 na 16.