
Hakuna uhusiano kati ya matumizi ya simu ya mkononi na
kuongezeka hatari ya kupata saratani ya ubongo, kulingana na uchambuzi mpya
uliofanywa kwa ajili ya Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), kwa kukusanya
ushahidi wa tafiti zilizochapishwa ulimwenguni.
Licha ya ongezeko kubwa la matumizi ya teknolojia ya simu,
hakujawa na ongezeko la matukio ya saratani ya ubongo, uchambuzi huo
uliochapishwa Jumanne umegundua. Hilo ni hata kwa watu wanaopiga simu kwa muda
mrefu au wale ambao wametumia simu kwa zaidi ya miaka kumi.
Uchambuzi huo wa hivi karibuni zaidi ulijumuisha tafiti
63 kutoka 1994-2022, zilizochambuliwa na wachambuzi 11 kutoka nchi 10, pamoja
na mamlaka ya ulinzi dhidi ya mionzi ya serikali ya Australia.
“Uchambuzi huo ulitathmini athari za masafa ya
redio, yanayotumiwa katika simu na vile vile TV, kamera za kufuatilia watoto na
rada,” anasema mhusika katika uchambuzi huo na profesa wa magonjwa ya
saratani katika Chuo Kikuu cha Auckland, New Zealand, Mark Elwood.
“Hakuna jambo kati ya mambo makuu yaliyochambuliwa
lililoonyesha hatari ya kupata saratani,” anasema.
Mapitio hayo yaliangalia saratani za ubongo kwa watu
wazima na watoto, na vile vile saratani ya tezi ya kuzalisha homoni katika
ubongo, tezi za mate na saratani ya damu, na hatari zinazohusiana na matumizi
ya simu, minara ya simu, vifaa vya kusambaza mawasiliano, pamoja na vifaa
vingine vinavyohusiana na simu.
Aina zingine za saratani zitaripotiwa katika uchambuzi
tofauti.
WHO na mashirika mengine ya afya ya kimataifa yamesema
hapo awali hakuna ushahidi wa uhakika wa madhara ya kiafya kutokana na mionzi
ya simu za mkononi, lakini ilitaka utafiti zaidi.
Kundi la ushauri la WHO limetaka uchambuzi huo
kuchapishwa upya haraka iwezekanavyo kutokana na taarifa mpya tangu tathmini
yake ya mwisho mwaka 2011. Tathmini hiyo ya WHO itatolewa katika robo ya kwanza
ya mwaka ujao.
Soma zaidi: