DRC yarefusha ushirikiano wa kijeshi na Uganda kupambana na waasi wa ADF

Rais Félix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amethibitisha uamuzi wa nchi yake ya kuendeleza ushirikiano wa kijeshi kati yake na Jeshi la Uganda UPDF katika vita dhidi ya waasi wa ADF huko Kivu Kaskazini na Ituri nchini DRC.

Uamuzi huu umekuja baada ya nchi hizo mbili kukaa na kutathimini kwa pamoja mafanikio ya ushirikiano wao wa kijeshi wa kupambana na waasi wa ADF.

Operesheni hizo za pamoja zilizoanzishwa mwezi Novemba 2021, zinalenga kuwasambaratisha wa Uganda ADF ambao wanatumia ardhi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kufanya mashambulizi ndani ya Uganda. 

Licha ya kuweko ushirikiano huo, Uganda inashutumiwa kuwaunga mkono waasi wa M23 wanaodaiwa kuungwa mkono pia na Rwanda suala ambalo limeleta mvutano kati ya Kinshasa na Kampala. Ripoti ya hivi karibuni ya Umoja wa Mataifa inadai kuwa Uganda imewasaidia viongozi wa waasi wa M23 kuitisha mkutano muhimu, suala ambalo limezua maswali kuhusu nia hasa ya Uganda ya kupeleka wanajeshi wake huko Kongo. 

Ni karibu miaka mitatu sasa imepita tangu Uganda ilipopelekea wanajeshi wake mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ili kushirikiana na jeshi la nchi hiyo kupambana na waasi wa ADF. Operesheni hizo za pamoja zilianza mwezi Novemba 2021 na zilipangiwa kufanyika kwa muda wa miezi sita. Ripoti mbalimbali zinaonesha kuwa majeshi ya nchi hizo yamefanikiwa kupunguza nguvu za waasi hao wa Uganda kiasi kwamba hivi sasa taarifa zinasema kuwa wamebakia kwenye vijikundi vidogovidogo wanaoshambulia wananchi kwa sura ya kuvizia chini ya jina hilo hilo la ADF.