DRC yapiga marufuku ndege za Rwanda kutumia anga yake

DRC imepiga marufuku ndege zote zilizosajiliwa nchini Rwanda au zilizopo nchini humo kutumia anga yake kutokana na vita vya uchokozi vinavyoendelea, Shirika la Habari la Kongo (ACP) limetangaza Jumanne.

Imechapishwa: Imehaririwa:

Dakika 1

Matangazo ya kibiashara

Uamuzi huu, uliochukuliwa na mamlaka ya anga ya Kongo, unafuatia ghasia mbaya ambazo zilisababisha vifo vya watu wasiopungua 3,000 katika muda wa siku nne huko Goma, kulingana na chanzo hicho.

“Marufuku rasmi ya kuruka na kutua katika viwaja vya ndege nchini  Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imewekwa kwa ndege yoyote ya kiraia na ya serikali iliyosajiliwa nchini Rwanda au iliyosajiliwa kwingine lakini ikiwa na makao yake nchini Rwanda, kutokana na hali ya ukosefu wa usalama inayohusishwa na vita,” inabaini hati ya ndani kutoka kwa mamlaka ya Kongo, iliyonukuliwa na ACP.

Hatua hii inajiri huku mvutano kati ya Kinshasa na Kigali ukiendelea kuongezeka. Mnamo Februari 8, Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika ya Kati (ECCAS) ililaani mashambulizi ya M23, kundi lenye silaha linaloungwa mkono na Rwanda, na kutaka kusitishwa mara moja kwa mashambulizi yake na kujiondoa katika maeneo inayoshikiliwa kimabavu huko Kivu Kaskazini.

Kwa upande wa kidiplomasia, Februari 5, Rais wa Baraza la Ulaya, António Costa, alibaini kwamba alizungumza na Marais Félix Tshisekedi na Paul Kagame kujaribu kutafuta suluhu la amani la mzozo wa usalama mashariki mwa DRC.

Afrika Kusini, kupitia serikali yake, ilithibitisha tena uungaji mkono wake kwa DRC mnamo Februari 3, licha ya ukosoaji kutoka kwa rais wa Rwanda ambaye alishutumu “upotoshaji” na “uongo” katika tafsiri ya mzozo huo.

Hata hivyo, Januari 25, DRC ilikataa pendekezo la upatanishi kutoka Uturuki, na kupendelea suluhu za Afrika kutatua mgogoro huo.