
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Felix Thisekedi, ameondoa adhabu ya kifo kwa raia watatu wa Marekani, waliokuwa wamehukumiwa kifo na sasa watafungwa maisha, kwa kuhusika kwa kile serikali ya Kinshasa ilieleza jaribio la mapinduzi mwaka uliopita.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Raia hao watatu, Marcel Malanga, Tyler Thompson na Benjamin Zalman-Polun wenye kati ya umri wa miaka 23 hadi 37, wamepata ahueni hiyo, wakati huu wakiendelea kuzuiwa kwenye Gereza la kijeshi jijini Kinshasa.
Watatu hao, walikuwa wamehukumiwa kifo baada ya madai ya kuhusika na jaribio la mapinduzi kwa kuvamia ofisi za rais jijini Kinshasa na makaazi ya Waziri wa uchumi wakati huo Vital Kamerhe, ambaye sasa ni spika wa bunge.
Jaribio la mapinduzi hayo, yaliongozwa na Christian Malanga, raia wa DRC aliyekuwa amepata uraia wa Marekani, ambaye alikuwa baba yake Marcel Malanga, aliuawa baada ya kupigwa risasi na maafisa wa usalama.
Richard Bondo, Wakili wa Zalman-Polun amefurahishwa na uamuzi wa rais Tshisekedi, hatua anayosema inatoa matumaini ya hatimaye kuachiwa huru.
Mwaka uliipita serikali ya DRC, iliondoa zuio la kisheria la kutekeleza adhabu ya kifo ambayo imekuwepo tangu mwaka 2003 ikiwalenga wanajesji wanaopatikana na makosa ya uhaini.
Tangu kipindi hicho, hukumu zaidi ya 100 ya vifo zimetolewa lakini hakuna aliyeuawa mpaka sasa.