DRC: Waasi wa M23 wauteka mji mpya kwenye mpaka na Uganda huku mazungumzo yakijivuta

Waasi wa M23 wanaendelea kupata nguvu mashariki mwa DRC.

Kundi hilo ambalo linaripotiwa kuungwa mkono na Rwanda liliuteka mji  huo wa kimkakati wa Kamandi Gîte,  siku ya Jumapili tarehe 3, kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari.

Kamandi Gîte iko kwenye kingo za Ziwa Edward na inaunganisha mji wa Beni.

Vyombo vya habari vya ndani vimenukuu vyanzo vya kuaminika nyanjani vikisema kwamba, wakazi wa eneo hilo walionekana wakikimbia kabla ya kuanguka mji huo mikononi mwa waasi.

Waasi wa M23 walikabiliana na wapiganaji wa kujilinda wanaojulikana kama Wazalendo ambao wanashirikiana na jeshi la DRC.

Mapigano hayo mapya yanakuja wakati wataalamu kutoka Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wakiendelea na mazungumzo ndani ya mfumo wa Mchakato wa Luanda.

Angola ni mpatanishi mkuu katika mazungumzo ya amani na  majirani hao.

Mkutano mwingine wa mazungumzo hayo  umepangwa kufanyika mnamo Novemba 16.

Rwanda na DRC zimeripotiwa kukubaliana juu ya mpango ambao utahusisha kutojumuishwa jeshini wapiganaji wa FDLR,  waliotekeleza mauaji ya kimbari ya  mwaka  1994 huko Rwanda.