Waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda wamechukua mji mwingine muhimu mashariki mwa DRC, siku mbili kupita tangu kundi hilo lisusie mazungmzo ya amani yaliyokuwa yafanyike mjini Luanda, Angola.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Mji uliodhibitiwa na waasi hao ni Walikale, wakazi kwenye eneo hilo wamethibtisha ambapo wameongeza kuwa kulikuwa na makabiliano kwa saa kadhaa.
Vyanzo vya kijeshi vimedai kuwa waasi hao walikuwa wakipambana na wanajeshi wa serikali pamoja na wanamgambo wanaoiunga mkono Kinshasa, hili likiwa shambulio la kushtukiza.
Mji wa Walikale, ambao uko katika eneo lenye utajiri mkubwa wa madini, ndio mji wa mbali zaidi kuelekea magharibi ambao umechukuliwa na M23 tangu walipoanza upya uasi wao.

Mji huo wenye takriban watu 15,000 upo umbali wa kilomita 125 kaskazini-magharibi mwa mji wa Goma, mji ambao waasi hao waliuteka mwezi Januari, na sasa wakibakia kilometa 400 tu kufika mji wa nne kwa ukubwa wa Kisangani.
Nchi jirani na mataifa ya kigeni zimekuwa zikiongoza juhudi za kidiplomasia ili kusitisha kile ambacho kwa haraka kimekuwa mzozo mbaya zaidi wa kibinadamu tangu vita vya mwaka 1998-2003 ambavyo vilihusisha mataifa kadhaa ikiwemo Angola na Zimbabwe.
Hatua ya waasi hawa kuchukua mji wa Walikale, inachukuliwa na wadadisi wengi kama kiburi kinachotokana na kuungwa mkono na Rwanda, waasi hao wakipuuza mwito wa kusitisha vita na kushiriki mazungumzo na Kinshasa.