DRC: Waasi wa AFC/M23 wadhibiti Kabamba na Katana na wanalenga uwanja wa ndege wa Kavumu

Waasi wa M23 sasa wako katika maeneo mawili y mko wa Kivu Kusini, ambayo ni maeneo ya Kalehe na Kabare, ambapo sasa wanakalia eneo la Kabamba na jiji la Katana. Maeneo muhimu yaliyo umbali wa kilomita saba, kulingana na vyombo vya habari nchini DRC.

Imechapishwa: Imehaririwa:

Dakika 1

Matangazo ya kibiashara

Kulingana na vyanzo vya ndani, mji wa Kabamba, unaopakana na eneo la Kalehe, umedhibitiwa na waasi baada ya mapigano yaliyoendelea hadi usiku wa Alhamisi, kabla ya jeshi kuondoka na kukimbilia Katana.

“Leo asubuhi mwendo wa saa 1:00 ndipo tulipopata taarifa kwamba Kabamba imeanguka mikononi mwa waasi wa M23. Na karibu saa 3:00 asubuhi, Katana pia imeanguka mikononi mwa waasi hao. Hakuna mkutano uliofanyika, wanawaambia watu waedelee na shughuli zao. Kulikuwa na mapigano huko Kabamba, pia na huko Katana lakini haikuchukua muda mrefu. Jeshi liliondoka kuelekea Kavumu kwenye uwanja wa ndege,” Gazeti la Actualite.cd limenuku moja ya vyanzo vyake ambacho hakikutaka kutajwa jina.

Chanzo kingine kinaongeza: “Mji wa Katana na Kabamba iko chini ya udhibiti wa waasi wa M23. Nadhani wanaelekea uwanja wa ndege wa Kavumu.”

“Kule Katana, waasi wapo, wanasalimia watu. Kwa sasa wapo Katana labda wanapumzika kabla ya kuendelea kuelekea uwanja wa ndege maana baada ya Katana ni Kavumu,” kimesema chanzo kingine kilichopo Katana.

Mapigano yamekoma katika maeneo yote mawili. Baadhi ya wakazi wameanza kujipanga kuondoka maeneo hayo kukimbilia Bukavu.

Waasi wa M23 wanaendelea na mashambulizi yao huko Kivu Kusini licha ya azimio la mkutano wa mwisho wa pamoja wa SADC-EAC uliofanyika Dar es Salaam, Tanzania, ambao ulipendekeza kusitishwa kwa mapigano mara moja. Wito kama huo ulitolewa, haswa na Umoja wa Ulaya, EU, kwa M23 kusitisha harakati zake na Rwanda kuondoa wanajeshi wake nchini DRC.