
Baada ya kumuua kiongozi wake katika shambulio la ndege isio na rubani katikati ya wiki, jeshi la Kongo limeshambulia tena kundi la kujilinda la Twirwaneho huko Kivu Kusini siku ya Ijumaa, Februari 21. Hasa, FARDC walianzisha mashambulizi yao dhidi ya wanamgambo hao katika eneo la Minembwe, eneo la nyanda za juu.
Imechapishwa:
Dakika 2
Matangazo ya kibiashara
“Mapigano katika wilaya ya kijijini ya Minembwe katika mkoa wa Kivu Kusini, yalianza mwendo wa saa 11 alfajiri siku ya Ijumaa, Februari 21, kimesema chanzo cha utawala katika eneo hilo kilichowasiliana na RFI. Kisha mapigano hayo yaliendelea kwa siku nzima, kati ya jeshi la Kongo (FARDC) na wanamgambo wanaoiunga mkono serikali (Wazalendo) dhidi ya wapiganaji wa kundi la kujilinda la Twirwaneho, ambalo kiongozi wake Michel Rukunda, almaarufu Makanika, afisa wa zamani wa FARDC wa cheo cha kanali aliyejiondoa katika jeshi hilo, aliuawa siku ya Jumatano, Februari 19 katika shambulio la ndege isio na rubani.
Ripoti ya hivi majuzi ya Umoja wa Mataifa inaelezea kundi la Twirwaneho kama “linashirikiana na muungano wa AFC/M23.” Kulingana na vyanzo kadhaa, kundi hilo linalojifanya mtetezi wa jamii ya Banyamulenge limekuwa likipambana dhidi ya jeshi la Kongo tangu mwaka 2020.
Siku ya Ijumaa, video zilizorushwa na wapiganaji wa kundi hili kwenye mitandao ya kijamii zinawaonyesha, pamoja na mambo mengine, mbele ya ofisi ya utawala ya wilaya ya Minembwe. Alipohojiwa alasiri na mwanahabari wetu mjini Kinshasa, Coralie Pierret, Luteni Marc Elongo, msemaji wa jeshi la FARDC katika eneo hili la Kivu Kusini, amethibitisha kuwa mapigano bado yanaendelea na kwamba bado ni mapema mno kubaini nani anadhibiti eneo hilo.
Huko Kinshasa, chaguo la mazungumzo labda linachukuwa mkondo wake
Ingawa, katika hatua hii, matarajio ya mapatano bado ni mbali na kuwa ukweli mashariki mwa DRC licha ya kuongezeka kwa wito wa kusitisha mapigano, ishara kadhaa zinaelekea kuonyesha kwamba wazo la mazungumzo labda linaanza kupata msingi miongoni mwa mamlaka za Kongo na kwamba Rais Félix Tshisekedi hajakataa kabisa kwa chaguo hili linalotetewa na wadau wengi wa ndani – na nje ya nchi. Luanda, Nairobi, Brazzaville na Pretoria, pamoja na Makanisa ya Kikatoliki na Kiprotestanti ya DRC, yanajaribu kuongeza mashauriano katika kujaribu kufikia suluhu la kisiasa.
Rasmi, bila shaka, mkuu wa nchi wa Kongo bado anashikilia msimamo wake, yaani: hakuna suala la kukubali mazungumzo ya moja kwa moja na AFC/M23. Lakini nyuma ya pazia, msimamo wake hauan tena nguvu na pia anafuatilia kwa karibu mpango unaoungwa mkono na Makanisa, vyanzo kadhaa vya karibu na rais vilimweleza mwandishi mwingine wa RFI katika mji mkuu wa Kongo, Patient Ligodi. Katika siku za hivi karibuni, Félix Tshisekedi alipokea washirika kadhaa wa kisiasa ambao walimtia moyo kuzingatia mfumo shirikishi zaidi wa majadiliano. Ukweli unabaki kuwa “ikiwa kutakuwa na mazungumzo, haitakuwa katika hali ambayo tuko kwa sasa”, anaeleza mmoja wa marafiki zake wa karibu ambaye anabainisha kuwa kabla ya kufikiria kuhusu hilo, “usawa fulani lazima uimarishwe kwanza”.