DRC: Majadiliano kati ya viongozi wa kidini na kiongozi wa zamani wa kivita Thomas Lubanga

Viongozi wa kidini kutoka Cenco na ECC wanaendelea na mashauriano yao katika kujaribu kutafuta suluhu la mzozo wa mashariki mwa DRC. Walikuwa nchini Uganda siku ya Jumanne wiki hii kwa mazungumzo na Rais Yoweri Museveni. Siku ya Jumanne jioni, pia walikutana na mbabe wa zamani wa kivita Thomas Lubanga. Alihukumiwa mwaka 2012 kwa uhalifu wa kivita na ICC na kisha kuachiliwa mwaka 2020, sasa anashutumiwa na Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na AFC-M23.

Imechapishwa:

Dakika 2

Matangazo ya kibiashara

Mkutano huo ulifanyika Kampala, ambako Thomas Lubanga anaishi tangu mwezi Julai 2024, kulingana na Umoja wa Mataifa. Mazungumzo yao yalikuwa mafupi. Hakuwa peke yake, lakini alizungukwa na msururu wa watu waliotoroka makazi yao kutoka Ituri, wakiwemo watu mashuhuri na wabunge wa zamani, ambao wako leo katika mzozo na mamlaka ya kijeshi ya mkoa huo.

Lengo la viongozi wa kidini: kuhamasisha Thomas Lubanga kwenye mpango wao unaoitwa “mapatano ya kijamii kwa ajili ya amani” na kumzuia kiongozi huyo wa zamani wa waasi kujihusisha kijeshi katika mzozo unaoendelea na kuchangia kuzorota kwake, huku shutuma dhidi ya Thomas Lubanga zikiongezeka.

Wiki iliyopita, mamlaka ya kijeshi huko Bunia ilimshutumu kwa kuanzisha kundi jipya la waasi, linaloshirikiana na M23. Kwa mujibu wa habari zetu, Thomas Lubanga anakanusha kuchukua silaha tena, lakini hafichi ukubwa wa malalamiko yake dhidi ya serikali iliyo madarakani.

Mwezi Januari, kundi la wataalamu wa Umoja wa Mataifa lilimshutumu kwa kuwa na “jukumu muhimu” katika kuunganisha kundi linalojihami la Zaire na AFC-M23 inayoungwa mkono na Rwanda. Amenyoshewa kidole cha lawama, kama sehemu ya “mamlaka ya kimaadili” ya kundi la Zaire, aliwezesha kuajiri wapiganaji, ikiwa ni pamoja na wapiganaji wa zamani wa kundi lake la UPC, na hata kuweka kambi za mafunzo huko Ituri na Uganda kwa msaada wa Rwanda.

Hali hii inayobadilika inawatia wasiwasi viongozi wa kidini zaidi kwani mapigano kati ya kundi la Zaire na maadui zake Codeco yameongezeka katika wiki za hivi karibuni, dhidi ya hali ya ushindani wa kikabila. Thomas Lubanga alipatikana na hatia ya mauaji ya mamia ya raia huko Ituri katika miaka ya 2000, wakati kundi lake la UPC liliposhirikiana na Uganda na kisha Rwanda.

Viongozi wa CENCO na ECC sasa wanapanga kwenda Angola, ambayo inashikilia urais wa zamu wa Umoja wa Afrika, kisha Zimbabwe, ambayo ni mwenyekiti wa SADC, na hatimaye Burundi.