
Wanajeshi wa M23 na Rwanda wanaendelea kusonga mbele katika mkoa wa Kivu Kusini, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Kulingana na msemaji wa jeshi la Kongo, wapiganaji wa M23 sasa wako Bukavu, mji mkuu wa mkoa, lakini hali bado ni tete.
Imechapishwa:
Dakika 2
Matangazo ya kibiashara
Siku ya Jumapili asubuhi, Februari 16, msemaji wa jeshi la Kongo alithibitisha kuwepo kwa wanajeshi wa M23 na Rwanda huko Bukavu, mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kusini. Wapiganaji wa kundi hili wapo katika maeneo kadhaa na haswa kwenye kituo cha mpaka na Rwanda, Ruzisi 1 na katika majengo ya serikali ya mkoa, anaelezea mwandishi wetu huko Kinshasa, Paulina Zidi.
Tangu Jumapili asubuhi, mashahidi wameeleza kuwa hali ni shwari katika jiji hilo. Kuna watu mitaani nashughuli zimerudi kama kawaida, lakini bado raia wana uoga. “Hali ni shwari, watu wanatembea, lakini kwa upande wangu napendelea kubaki nyumbani,” anasema mkazi mmoja.
Kinshasa inashtumu M23 kushikilia miji mikuu ya mikoa ya Kivu Kaskazini na Kusini. “Bukavu, Goma na maeneo mengine yote yanayokaliwa kwa mabavu katika mikoa ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini ni alama ya upinzani wetu,” ilitangaza Wizara ya Mawasiliano siku ya Jumapili mchana, na kuongeza kuwa “kinyume na maazimio ya Dar es Salaam, kwa wito wa kusitishwa mapigano kutoka kwa jumuiya ya kimataifa, Rwanda inaendelea na mpango wake wa uvamizi, uporaji, uhalifu na ukiukwaji wa haki za binadamu.” Kinshasa inaendelea kutoa wito wa kuwekewa vikwazo jirani yake.
Siku ya Ijumaa jioni, chanzo cha serikali ya Kongo kilietaja kuingia kwa kundi hilo lenye silaha katika mji wa Bukavu. Lakini siku ya Jumamosi, habari hiyo ilikuwa ya kutatanisha sana. Matukio ya uporaji yaliripotiwa. Mapema jioni, askari wa FARDC walionekana tena mjini, habari iliyoripotiwa katika taarifa kutoka ofisi ya rais ambayo iliitisha kikao cha baraza la usalama wa taifa Jumamosi jioni. Usiku wa Jumamosi kuamkia Jumapili, milio ya risasi ilisikika hadi kwenye mpaka na Rwanda.
Kufikia sasa idadi ya vifo haijulikani. Kulingana na mkuu wa ujumbe wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) inayounga mkono hospitali kuu ya mkoa, watu waliojeruhiwa katika vita, waliojeruhiwa kwa risasi na waliojeruhiwa kwa milipuko walilazwa Jumamosi na Jumapili katika hospitali hiyo. Hali ya utulivu siku ya Jumapili iliruhusu misheni ya upelelezi katika jiji hilo ambapo miili ya watu waliouawa ilionekana. Timu za shirika la Msalaba Mwekundu zinatumai kuweza kuondoa leo maiti hizokama tahadhari ya kiafya na kujaribu kuwatambua na kuwafanyia mazishi.