
Waasi wa M 23 wanaoungwa mkono na Rwanda, wamekaribisha kwa masharti tangazo la Angola, kushiriki kwenye mazungumzo na serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ili kumaliza mzozo wa Mashariki mwa nchi hiyo.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Kupitia taarifa yao, waasi hao wamesema watakuwa tayari kushiriki kwenye mazungumzo hayo yanayotarajiwa kufanyika jijini Luanda.
Hata hivyo, waasi hao wametoa sharti kwa rais Felix Thisekedi atangaze hadharani kuwa, atashiriki kwenye mazungumzo hayo.
Rais Tshisekedi, katika kipindi cha nyuma, amekuwa akigoma kuzungumza na waasi hao, akiwaita magaidi.
Msemaji wa rais Tshisekedi Tina Salama, kupitia ukurasa wake wa X, amesema, serikali ya DRC, inatambulia jitihada za Angola, lakini hakueleza iwapo kiongozi wa nchi hiyo atashiriki.
Angola, ambaye ni mpatanishi wa mzozo wa DRC siku ya Jumanne, ilitangaza kuwa kuwa, mazungumzo hayo ya moja kwa moja, yataanza Machi 18.
Mwezi Desemba mwaka 2024, Angola iliandaa mazungumzo kati ya rais Thisekedi na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame.
Mazungumzo hayo yalivunjika baada ya kiongozi huyo wa Rwanda kutokwenda Angola.