Mahakama ya kijeshi jijini Kinshasa imeanza kusikiliza kesi dhidi ya maofisa wa juu wa jeshi FARDC waliokimbia maeneo yao ya kazi wakati waasi wa M23 wanaosaidiwa na Rwanda walipovamia miji ya Goma na Bukavu.
Imechapishwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Majenerali watano wakiwemo wawili wa polisi na watatu wa jeshi la FARDC, ndio walikuwa mbele ya mahakama kuu ya Kijeshi. Miongoni mwao ni pamoja na makamu gavana wa Kivu Kaskazini Jenerali Ekuka Lipopo, Kamanda wa eneo la 34 la kijeshi Alengbia Nyitetesya, kamanda wa Brigadi la 11 huko Sake, Kamishna wa Polisi wa Mkoa wa Kivu Kaskazini na mshauri wa gavana anayesimamia usalama na utaratibu wa umma.
Wote hawa, wanatuhumiwa kwa kuonyesha “uoga”, kupoteza vifaa vya kijeshi, silaha na risasi, kuchochea askari kufanya vitendo kinyume na sheria, uvunjaji wa amri pia kukimbia adui na kuteka boti ya kibinafsi ya mfanyabiashara Vanny Bishweka na kuwaacha maofisa wao bila amri.

Wameshtakiwa kwa mujibu wa kifungu cha 36 na 68 za kanuni za kijeshi, kwa mujibu wa mwendesha mashtaka.
Kwa kesi hii, mahakama kuu ya kijeshi itahukumu tu majenerali waliotumwa Goma huko Kivu Kaskazini na kesi imepangwa tena kusikilizwa tarehe ishirini mwezi huu.
Freddy Tendilonge/Kinshasa/ RFI Kiswahili