
Rais wa Zamani wa DRC Joseph Kabila ambaye anakabiliwa na shutuma kali kadhaa – uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya ubinadamu na mauaji ya raia – nchini DRC, anaimarisha mtandao wa washirika wake. Kwa takriban mwaka mmoja, rais huyo wa zamani wa Kongo amekuwa akifanya mikutano mingi katika kanda hiyo.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Amekutana na wakuu wa sasa wa nchi, pamoja na viongozi wa zamani wa Afrika. Joseph Kabila ametuma barua kwa baadhi yao ambapo anashiriki uelewa wake kuhusu hali ya kisiasa nchini DRC na mzozo wa usalama katika eneo la Maziwa Makuu. Tangu mwanzoni mwa mwaka huu, amezuru Nairobi ambapo alikutana na Rais wa Kenya William Ruto. Maudhui ya mazungumzo yao hayajawekwa wazi.
Siku nne zilizopita, alikuwa na mkutano wa moja kwa moja na Olusegun Obasanjo, rais wa zamani wa Nigeria, mwezeshaji mwenza aliyeteuliwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki na SADC. Majadiliano hayo yalichukua muda wa saa moja. Obasanjo, ambaye pia anadumisha uhusiano na Rais wa Kongo Félix Tshisekedi, alikuwa amezungumza muda mfupi kabla na Massad Boulos na alisafiri hadi Qatar kukutana na wapatanishi wa Qatar.
Katika ngazi ya kitaifa, Joseph Kabila hivi karibuni alikutana na viongozi wa upinzani. Kwa mara ya kwanza, alisaini taarifa ya pamoja na Martin Fayulu. Pia aliendelea kuwasiliana na Moïse Katumbi. Wote wawili wanatoka Katanga. Kwa pamoja, wanatetea zaidi kuandaliwa kwa mchakato wa mazungumzo ya kitaifa nchini Kongo ili kushughulikia sababu kuu za mgogoro wa pande nyingi ambao nchi inapitia. Pia wanaunga mkono mpango wa mazungumzo unaohimizwa na madhehebu ya kidini, hasa Makanisa ya Kikatoliki na Kiprotestanti.