DRC : Joseph Kabila aanzisha mazungumzo na wanasiasa wa upinzani

Rais wa zamani wa DRC, Joseph Kabila ameanzisha mazungumzo na wanasiasa wa upinzani kuhusu mustakabali wa kisiasa wa nchi hiyo, wakati huu waasi wanaoungwa mkono na Rwanda wa M23 wakiendelea kushikilia miji kadhaa ya mashariki mwa nchi hiyo, vyanzo kadhaa vya karibu vimethibitisha.

Imechapishwa: Imehaririwa:

Dakika 2

Matangazo ya kibiashara

Majadiliano hayo, ambayo pia yamehusisha wanachama wa mashirika ya kiraia, yanaongeza shinikizo zaidi kwa Rais Felix Tshisekedi ambaye anakabiliwa na ukosolewaji mkubwa kwa namna anavyoshughulikia mzozo unaoendelea mashariki mwa nchi yake.

Tshisekedi na Kabila, wakati mmoja waliwahi kufanya kazi pamoja ambao vyama vyao vilisaini makubaliano ya kugawana madaraka kufuatia uchaguzi wa mwaka 2018 uliokumbwa na utata, makubaliano ambayo hata hivyo baadae yalianza kupuuzwa na Tshisekedi akimshutumu mtangulizi wake kwa kuzuia mageuzi.

Rais wa DRC Félix Tshisekedi, Tarehe 14 2025 akiwa mjini Munich.
Rais wa DRC Félix Tshisekedi, Tarehe 14 2025 akiwa mjini Munich. © Michaela Stache / AFP

Uhusiano wa wawili hao ulidorora kiasi kwamba, wakati waasi wa M23 walipoamua kuelekea mji wa Bukavu mwezi uliopita, Tshisekedi aliuambia Mkutano wa Usalama wa Munich kwamba Kabila ndiye aliyefadhili uasi.

Kabila hakutoa tamko lolote la hadharani kuhusu mgogoro huo au kujibu shutuma hizo hadi alipochapisha tahariri katika gazeti la Afrika Kusini Februari 23 ambapo alimshutumu Tshisekedi kwa kukiuka katiba, kutekeleza vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu na kuifikisha Kongo kwenye ukingo wa vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Joseph Kabila alituhumiwa na rais Felix Thisekedi kwa kufadhili waasi
Joseph Kabila alituhumiwa na rais Felix Thisekedi kwa kufadhili waasi © Jerome Delay / AP

Aidha Vyanzo zaidi vinadai kuwa, wakati Kabila na wajumbe wake walikuwa wamezungumza kuhusu aina fulani ya mpito wa kisiasa, hakukuwa na mpango wazi au maelezo ya kina kuhusu wanachokitarajia toka kwenye majadiliano yao.

Mazungumzo hayo yamekuwa ya faragha, ingawa Kabila alikutana kwa uwazi mwezi Desemba mjini Addis Ababa na viongozi wa upinzani Moise Katumbi na Claudel Lubaya.