DRC: Hofu yatanda kwa wakaazi wa mji wa mpakani wa Uvira kufuatia kusonga mbele kwa M23

Milio ya risasi ilisikika katika mji wa Uvira, mji ulio kwenye mpaka na Burundi, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo siku ya Jumatano, duru za ndani zimesema, wakati mapigano yakizuka kati ya vikosi vya serikali na washirika huku waasi wanaoungwa mkono na Rwanda wakisonga mbele.

Imechapishwa:

Dakika 3

Matangazo ya kibiashara

Wakazi na maofisa wameeleza matukio ya uporaji, maiti zikiwa mitaani na askari wa serikali wakijaribu kutumia boti kutoroka kupitia Ziwa Tanganyika. Wafungwa katika jela la Uvira wametoroka, kulingana na vyanzo hivyo vilivyonukuliwa na shirika la habari la REUTERS.

Waasi wa M23 wamekuwa wakielekea kusini kuelekea Uvira, mji ambao unashiriki ziwa moja na Burundi, tangu kuteka mji mkuu wa mkoa wa Bukavu mwishoni mwa wiki hii – hasara kubwa zaidi kwa Kongo tangu kuanguka kwa mji mkubwa wa eneo hilo, Goma, mwishoni mwa Januari.

Kuingia kwa wapiganaji wa M23 hao katika mji wa Kamanyola siku ya Jumanne kulizua hofu huko Uvira, kilomita 80 kusini mwa DRC. Tangu kuanguka kwa mji wa Bukavu, wanajeshi wa Kongo wanaorudi nyuma wamejikuta wakipambana na wanamgambo washirika, Wazalendo, ambao hawataki kusalimu amri mbele ya M23.

“Tuliamka risasi zikirushwa kwa sababu ya kusonga mbele kwa waasi, ambao bado wako mbali,” afisa wa eneo hilo amesema, akizungumza kwa sharti la kutotajwa.

“Vikosi tulivyokuwa tunavitegemea, FARDC (jeshi la serikali) na Wazalendo, wako migogoro. Vifo vimeripotiwa na uporaji. “

Wakazi wanne wa Uvira pia wamesema wamesikia milipuko ya risasi katika mji huo. Chanzo cha misaada ya kibinadamu kimesema kimeona miili kadhaa mitaani, takriban miili 30 katika chumba cha kuhifadhi maiti cha jiji hilo na zaidi ya watu 100 wamelazwa hospitalini wakiwa na majeraha mabaya kufuatia ghasia hizo. Shirika la habari la REUTERS halikuweza kuthibitisha kwa uhuru takwimu hizo.

Machafuko hayo yanasisitiza kudhoofika kwa udhibiti wa mamlaka za Kongo mashariki, ambapo mafanikio makubwa ya M23 katika eneo na kuteka maeneo yenye thamani ya uchimbaji madini kumezusha hofu ya vita vikubwa zaidi.

Wanajeshi wengi walijazana kwenye boti wakijaribu kutoroka mji wa Uvira, chanzo cha usalama kimesema, na kuongeza kuwa hali hii “ilizua machafuko kati ya watu ambao walitarajia kupanda boti kwa ajili ya usalama wao,” wakati “risasi zilikuwa zikirushwa pande tofauti.”

Wafungwa waachiliwa

Wafungwa, wakiwemo askari 228 ambao walikuwa wamekamatwa kwa kutoroka wameachiliwa kutoka gereza la eneo hilo, chanzo cha usalama kimesema. Haijulikani ikiwa wafungwa hao walilazimisha kutoka gerezani au waliachiliwa.

Matumaini kwamba Kongo inaweza kujilinda dhidi ya M23 yamefifia baada ya kuondolewa hivi karibuni kwa wanajeshi washirika wa Burundi, vyanzo vililiambia shirika la habari la REUTERS siku ya Jumanne. Burundi imekanusha kuondoa wanajeshi wake.

Wakati huo huo, mapigano kati ya waasi na jeshi la Kongo pia yamezuka katika mkoa jirani wa Kivu Kaskazini, msemaji wa jeshi Mak Hazukay amesema siku ya Jumatano, akiongeza kuwa baadhi ya wanajeshi wametelekeza ngome zao katika eneo hilo, jambo linalozua hofu.

Kundi la M23 lililo na vifaa vya kutosha ndilo la hivi punde katika safu ndefu ya vuguvugu la waasi wanaoongozwa na Watutsi kuibuka mashariki mwa Kongo, na kuibua upya mzozo wa mamlaka, uhasama wa kikabila na rasilimali za madini ambao ulianza miaka ya 1990 aada ya mauaji ya kimbari katika nchi jirani ya Rwanda.

Rwanda inakanusha madai ya Kongo na Umoja wa Mataifa kwamba inasaidia kundi hilo kwa silaha na wanajeshi. Inasema anajilinda dhidi ya wanamgambo wa Kihutu, ambao wanasemekana wanasaidia jeshi la Kongo.

Congo inakataa malalamiko ya Rwanda na kusema Rwanda imetumia wanamgambo wake kupora madini yake kama vile coltan, inayotumika katika simu za kisasa na kompyuta.

Machafuko ya mashariki yamechochea hali ya wasiwasi na hofu umbali wa maili 1,000 kutoka mji mkuu Kinshasa, ambapo baadhi ya wakaazi wanatafuta kuhamisha familia zao huku kukiwa na mazungumzo ya wazi ya mapinduzi.