DRC: FARDC yawataka wanajeshi watoro kujiunga na vikosi vyao, hofu yatanda Lubero

Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, FARDC, siku ya Alhamisi limewataka wanajeshi waliokimbia mashambulizi ya M23 kuungana tena na vikosi vyao na kusaidia kuzuia hasara zaidi katika nchi yao.

Imechapishwa:

Dakika 1

Matangazo ya kibiashara

Wakazi wa Lubero, takriban kilomita 250 kaskazini mwa mji mkuu wa jmko wa Kivu Kaskazini, Goma, wameliambia shirika la habari la AFP kwamba makundi ya wanajeshi wa Kongo yalikuwa yakipora mji wa Lubero wakati M23 ilipokuwa ikikaribia mji huo.

“Natoa wito kwa askari wote ambao wametoroka katika uwanja wa mapigano na ambao huranda randa Lubero na viunga vyake kurejea kwa makamanda wao,” Kanali Mak Hazukay, msemaji wa jeshi katika mkoa huo, amesemakatika ujumbe uliotangazwa kwenye redio zinazopeperusha matangazo yao katika eneo hilo.

“Askari hapaswi kumuacha mkuu wake na kundi lake.”

Mwandishi wa habari kutoka Lubero, ambaye ameomba jina lake lisitajwe kwa sababu za kiusalama, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba “askari waliokimbia walifyatua risasi katikati ya mji” na “kupora maduka na makampuni”.

Wakaazi kadhaa waliowasiliana na shirika la habari la AFP walithibitisha matukio hayo.

Aline Nyota anasema alikuwa akisafiri kutoka Lubero kwenda Butembo, kilomita 45 zaidi kaskazini, wakati “askari wa Kongo tuliokutana nao walipotuibia: simu, pesa na bidhaa zingine”.

“Ikiwa unasita, wanakupiga risasi,” amesema.

Mwandishi wa habari wa eneo hilo amesema wanajeshi wa Uganda wakisaidiwa na vifaru walikuwa wakishika doria Lubero ili kuhakikisha usalama.

Vikosi vya M23, vinavyoungwa mkono na wanajeshi wa Rwanda kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, vimepata upinzani mdogo tangu kutwaa Goma Januari 28.

“Ni juu yetu kupambana, kurejea kwenye ngome zetu na kufanya kazi,” Kanali Hazukay amesema, akiwasihi wanajeshi watoro kutowadhulumu raia.