
Jeshi la serikali ya jamhuri ya kidemokrasia ya Congo limesema kwamba limefanikiwa kuudhibiti upya mji wa kimakakati wa Walikale wenye zaidi ya wakazi 60,000 tangu jana huko Kivu Kaskazini, mashariki mwa nchi hiyo; baada ya kuondolewa kwa waasi wa M23/AFC, Wanaoungwa mkono na Rwanda.
Imechapishwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Kwa mujibu wa mashuhuda ambao ni wakaazi wa mji huo wa Walikale ni kuwa watu walishangazwa siku ya Jumatano kuona waasi hao wa M23 wanaosaidiwa na jeshi la Rwanda RDF wakijiondoa katika ngome zao zote walizokuwa wamedhibiti.
Hatua hii imethibitishwa na mkaazi huyu aliyewasiliana nasi baada ya kutafuta sehemu yenye kuwa na mtandao wa simu…. Aliomba jina lake libanwe kwa sababu za kiusalama.
“Ni siku ya jumatano ndio tulitambua kwamba hawako tena hapo, tulizunguuka katika kambi zao zote tuliona kwamba walikuwa wameondoka, ni vigumu kueleza sababu hakuna mtu ambaye alijua kwamba wataondoka; walikuwa maeneo ya karibu na hospitali majira ya jioni lakini hakuna aliyejua kwamba wataenda kila mtu alishangaa kuona wameenda. Kuonekana tena kwa FARDC mjini ni ahueni kwa sababu kulikuwa uporaji, na waliposikia waasi wameenda, ndiposa askari wetu walikuja tena mjini walikale na watu wameanza kurudi tena manyumabni kwao. Ni matumaini kwamba mambo yataendelea hivyo.” alisema mmoja walioshuhudia.
Mji huo wa walikale ulioko kilomita 400 zaidi kaskazini kuelekea Kisangani, mji mkuu wa mkoa wa Tshopo, ulianguka mikononi mwa kundi la waasi wa M23 wiki mbili zilizopita.
Walikuwa wamezingirwa na jeshi la Congo FARDC na wazalendo, ambapo msemaji wa jeshi la serikali anasema walijiondoa kutokana na shinikizo walilopewa.
Lakini upande wa waasi wa M23 wao wanasema katika tangazo lao kwamba wamejiondoa huko walikale, ili kutoa nafasi ya mazungumzo yanayopangwa kufanyika Aprili Tisa huko Doha Qatar, kati yao na serikali ya Kinshasa.