
Serikali ya DR Congo na Umoja wa Mataifa inaomba wahisani Dolla Bilioni 2.54 kwa ajili ya misaada ya kibinadamu mwaka huu.
Imechapishwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Ombi hili limekuja wakati huu mamilioni ya watu nchini DRC wakiwa waathiriwa wa vita, magonjwa na majanga ya asili.
Upatikanaji wa fedha hizo, umeelezwa kuwa muhimu kuwezesha utoaji wa misaada kwa watu Milioni 11, wakiwemo wakimbizi wa ndani Milioni 7.8.
Bruno Lemarquis, Mratibu wa Umoja ya Mataifa kuhusu misaada ya kibinadamu nchini DRC, amesema fedha hizo zitasaidia kupatikana kwa mahitaji muhimu kuwaisaida watu wanaohangaika kote nchini humo.
Mwaka huu pekee, Umoja wa Mataifa umepanga kuwafikia watoto zaidi ya Milioni 1.5 wanaokabiliwa na tatizo la utapia mlo, kuhakikisha kuwa watu wengine Milioni tano wanapata maji safi, na kukabiliana na mlipuko wa magonjwa kama Mpox na kipindupindu.
Wito huu unakuja wakati huu Mashariki mwa DRC kukishuhudiwa waasi wa M 23 wakidhibiti miji ya Goma na Bukavu, hali ambayo imetatiza shughuli za kawaida, ikiwemo upatikanaji wa mahitaji muhimu, kama chakula.