
Makanisa ya Kikatoliki na Kiprotestanti nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) yanaendelea na ziara yao ya mashauriano kuandaa mazungumzo. Baada ya Kinshasa, Goma, Kigali, Nairobi na bara la Ulaya, ni zamu ya Lubumbashi, katika mkoa wa Haut-Katanga (kusini-mashariki), kupokea wajumbe wa Baraza la Kitaifa la Maaskofu wa Kongo (CENCO) na Kanisa la Kristo nchini Kongo (ECC).
Imechapishwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Na mwandishi wetu mjini Lubumbashi, Joseph Kahongo
Baada ya misa ya ufunguzi wa mkutano iliyofanyika siku ya Alhamisi, Februari 20, viongozi wa kidini walipokea, katika dayosisi kuu ya Lubumbashi, wawakilishi wa mashirika ya kiraia, wafanyakazi wa kisiasa na viongozi wa kimila kutoka mikoa minne ya kusini mashariki inayojulikana kama “eneo la Grand Katanga.”
Ili kushiriki katika mashauriano ya kijamii ya amani, wajumbe wa mashirika ya kiraia katika eneo la Katanga wameweka masharti yao: “Hatupaswi kujadili kukiukwa kwa mipaka. Nchi ni moja na bado haijagawanyika. Pili, wale ndugu zetu wa Katanga waliokamatwa waachiliwe kabla ya mkutano huu. Tatu, walio uhamishoni pia waweze kurejea nchini mwao. Na nne, mazungumzo haya lazima yawe jumuishi, ni kusema, sio tu kushughulikia maswala ya kisiasa, bali pia maswala ya mgawanyo wa mapato. “
Mtazamo wa mazungumzo wa CENCO na ECC – uliokosolewa mahali pengine – juu ya ukweli wa kutaka kujumuisha hata waasi wa AFC/M23, unapokelewa vyema na vijana, kusini-mashariki mwa DRC, waliojumuishwa katika muundo wa Vijana kwa Umoja wa Katanga: “Historia ya nchi inatufundisha kwamba wakati Kanisa linasimama kwa kujitolea kurejesha amani nchini, sisi daima tunatafuta njia ya kuondokana na mgogoro. “
Askofu Donatien Nshole, katibu wa CENCO, anasema mkabala huu wa mazungumzo unahalalishwa kwa kiasi kikubwa: “Ni suala la Wakongo kukutana kwenye meza ili kuondoa tofauti zao, ili kupata mwafaka wa kitaifa, si kuhusu kugawana madaraka, lakini badala yake tafakari ambazo zingeongoza kwenye msingi imara wa ujenzi upya wa taifa. “
Baada ya Lubumbashi, mashauriano yanaweza kuendelea nchini Angola na Congo-Brazzaville, hasa.