
Tangu Februari 14, wakati waasi wa M23/AFC wanaoungwa mkono na Rwanda walipojaribu kudhibiti mji wa Bukavu, mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kusini, karibu Wakongo 10,000 waliotoroka wakihofia kuuawa na waasi wamepokeewa nchini Burundi, serikali ya Gitega inasema.
Imechapishwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Serikali ya Burundi inaeleza kwamba Wakongo hao “huingia kupitia mpaka rasmi wa Gatumba au kwa kuvuka Mto Rusizi katika mikoa ya Bubanza na Cibitoke”, na kupelekwa kwenye vituo vya kupokea wakimbizi vya Gihanga (mkoani Bubanza) na Cibitoke kwa ajili ya kutambuliwa na kutenganishwa kulingana na mahitaji yao maalum, kama vile kijeshi, raia, wagonjwa, watoto n.k.
Burundi inahakikisha kuwa inashirikiana kwa karibu na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) kutatua matatizo yanayohusiana na mapokezi ya watu hao wanaotoroka nchi yao.
Katika jiji la Bukavu, lililotekwa na waasi, maisha bado hayajarejea kuwa ya kawaida. Tangu Ijumaa iliyopita, shughuli zote zimekwama kutokana na uporaji uliofuatia kuondoka kwa Vikosi vya Wanajeshi wa Kongo katika mji huo wakati waasi walikuwa wakipiga kambi huko Kavumu.
Siku ya Jumatatu, Bukavu ilionekana kama jiji lisilo na shughuli. Shughuli zote zimesimama. Maduka na madukayamefungwa huku mengi yakiwa yameporwa, milango iko wazi. Jiji ni chafu, na takataka na vifusi vya bidhaa zilizoporwa vinaonekana mitaani kote.
Wakazi wamejificha kwenye nyumba zao. Shule hazijafungua milango yao. Ni teksi na pikipiki chache tu ndizo zilizoonekana mwanzoni mwa juma. Katika taarifa yake Jumapili iliyopita, serikali iliishutumu Rwanda kwa kukataa kuheshimu mahitimisho ya mkutano wa hivi karibuni wa pamoja wa EAC-SADC. Serikali ya Kinshasa ilitoa wito kwa wakazi wa Bukavu kukaa salama, ikiongeza kuwa miji ya Bukavu na Goma, pamoja na maeneo yote yanayokaliwa katika mikoa ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini, yanasalia kuwa ishara ya upinzani wa Kongo.