DRC: Baadhi ya vyama vya kisiasa vyasusia majadiliano ya kitaifa

Vyama kadhaa vya upinzani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) vimesusia mashauriano ya kisiasa yenye lengo la kuunda serikali ya umoja wa kitaifa yaliyoanzishwa na Rais Félix Tshisekedi, Jijini Kinshasa.

Imechapishwa: Imehaririwa:

Dakika 1

Matangazo ya kibiashara

Kinachoendelea jijini Kinshasa huko DRC ni kuwa baada ya kurejelewa kwa mashauriano hayo ya kisiasa hapo jana siku ya jumatatu Wanasiasa wa upinzani walizungumza na vyombo vya habari vya ndani, na kusema kwamba mbinu ya Rais Tshisekedi haitasuluhisha mzozo wa sasa wa usalama lakini badala yake mbinu hiyo itaimarisha serikali ya bwana Tshisekedi ambayo inakumbwa na mzozo wa kiutawala.

Wapinzani wanadai kuwa hawataunga mkono kile wanachoelezea kama siasa za nyuma ya pazia wakiushutumu utawala kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake kwa raia na Badala yake, wanaunga mkono mpango wa mazungumzo jumuishi, kama ilivyopendekezwa na maaskofu wa Baraza la Kitaifa la Maaskofu wa Kongo (CENCO) na wachungaji wa Kanisa la Kiprotestanti nchini Kongo (ECC), kutoa suluhu la kudumu kwa mzozo wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Martin Fayulu, kiongozi wa upinzani nchini DRC ni miongoni mwa wanasiasa ambao wamesusia majadiliano hayo ya kitaifa.
Martin Fayulu, kiongozi wa upinzani nchini DRC ni miongoni mwa wanasiasa ambao wamesusia majadiliano hayo ya kitaifa. REUTERS – Baz Ratner

Vyama vya kisiasa kama ECIDE chama kinachoongozwa naye Martin Fayulu, na kile cha “Ensemble pour la République,” kinachoongozwa na Moise Katumbi, ni miongoni mwa wale wanaokataa kushiriki katika mchakato mwingine wowote wa mazungumzo sambamba na mpango wa maaskofu.

Wote wanamtaka Félix Tshisekedi kuacha ujanja wa kisiasa na kuweka masilahi ya watu juu ya matarajio yake, huku muungano wa FCC, familia ya kisiasa ya Rais wa zamani Joseph Kabila, ikihoji ulazima wa mpango huu mpya wa serikali ya DRC.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *