
Takriban wanajeshi 200 waliotumwa na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) waliondoka katika mji wa Goma mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo siku ya Jumatatu, Februari 24. Wanajeshi waliosalia wa Afrika Kusini, Malawi na Tanzania wamesalia katika kambi yao huko Goma, jiji ambalo sasa linadhibitiwa na kundi la AFC/M23 linaloungwa mkono na Rwanda.
Imechapishwa:
Dakika 2
Matangazo ya kibiashara
Na mwanahabari wetu mjini Kinshasa, Coralie Pierret
Wanajeshi hawa wa SADC walietumwa tangu mwezi Desemba 2023 mashariki mwa DRC, kwa msaada wa jeshi la Kongo na kuzuia kusonga mbele kwa M23.
Wanajeshi waliojeruhiwa, wagonjwa na baadhi ya wafanyakazi wa kike waliondoka katika vituo vyao na hospitali huko Goma siku ya Jumatatu asubuhi, Februari 24, kuelekea kituo cha mpakani cha Grande Barrière, kisha uwanja wa ndege wa Kigali, mji mkuu wa Rwanda, na kurejea katika nchi zao.
Kwa jumla, “askari 194” kutoka SAMIDRC, ujumbe uliotumwa na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika, kulingana na AFC/M23. “Chini kidogo ya 200,” kinathibitisha chanzo cha kijeshi cha Kongo.
AFC/M23 imewataka wanajeshi wote wa kigeni waliopo katika eneo hilo kuondoka. Kwa sasa, wanajeshi wengine wa Afrika Kusini, Malawi na Tanzania ambao idadi yao kamili haijafahamika, bado wamezuiliwa katika kambi zao katika uwanja wa ndege na Mubambiro, nje kidogo ya mji wa Goma, wakiwa na silaha zao. “Kwa sasa tunafanya mazungumzo ya kuondoka kwao,” imesema AFC/M23.
Afrika Kusini, kwa upande wake, kulingana na vyanzo kadhaa vilivyotumwa mapema mwezi Februari, ina wanajeshi na zana za kijeshi huko Lubumbashi, moja ya miji mikubwa mashariki mwa DRC, zaidi ya kilomita 1,500 kusini mwa ukanda unaodhibitiwa na M23, madai ambayo jeshi la Afrika Kusini halijathibitisha. Mnamo mwezi wa Januari, Afrika Kusini ilipoteza wanajeshi kumi na wanne katika vita vya Goma.
Kambi za MONUSCO zimejaa watu kupita kiasi
Wanajeshi wengi wa Kongo pia wamekwama katika kambi za Goma, zile za Umoja wa Mataifa baada ya kupata hifadhi katika kambi hizo mwishoni mwa mwezi Januari. Kuna zaidi ya watu 1,400 kati yao kulingana na Umoja wa Mataifa, wengi wao wakiwa wanajeshi wa Kongo, wanamgambo wachache wanaoiunga mkono serikali, Wazalendo, raia wachache wakiwemo wanawake na watoto. “Hali ya sasa si endelevu kutokana na idadi kubwa ya watu walio chini ya ulinzi wetu,” kimesema chanzo cha Umoja wa Mataifa. MONUSCO inataka suluhu la dharura kuwatoa watu hawa na kuwapeleka mahali salama. Kwa upande wake, AFC/M23 inakusudia kuwajumuisha wanajeshi hawa katika kundi lao, isipokuwa kwa wale wanaotaka kurejea maisha ya kiraia, imebainishwa.