Drake kutumbuiza kombe la dunia 2026

Marekani. Baada ya kutolewa kwa taarifa kuwa kutakuwa na burudani wakati wa mapumziko kwenye Fainali za Kombe la Dunia mwakani, sasa Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Gianni Infantino ameonesha nia ya kumtaka Drake kutumbuiza katika mchezo huo.

Wakati alipokuwa kwenye mahojiano ya ‘Good Day New York’ na Mtangazaji Rosanna Scotto ambaye alimshauri Infantino kumchukua rapa huyo kutoka Canada ili kurudisha mashambulizi kwa Kendrick Lamar, ambaye alitumbuiza kwenye Super Bowl LIX.

“Nina wazo zuri kwa ajili yako kwa ajili ya halftime, unaweza kumchagua Drake kwa sababu Kendrick Lamar alimkashifu kwenye Super Bowl,” alisema mtangazaji huyo.

Hata hivyo, Infantino alijibu na kusema:  “Hivyo tunaweza kuunda aina fulani ya ushindani?, hilo ni wazo zuri kwa kweli Drake alikuwa pamoja nasi tulipotangaza wenyeji wa mashindano hayo, nadhani nimehifadhi namba yake mahali fulani nitamtafuta.”

Kupitia mitandao ya kijamii mashabiki walijibu na kuzua mijadala kuwa onyesho la Drake kwenye Kombe la Dunia litakuwa bora na kubwa kuliko onyesho la Kendrick Lamar kwenye Super Bowl, huku wengine, hasa Wamarekani, wakipuuza wazo hilo.

Ingawa onyesho la Drake halijathibitishwa, Chris Martin na Phil Harvey wa Coldplay wameteuliwa kuwa wasimamizi wa Halftime Show ya kwanza kabisa ya Kombe la Dunia, ambayo inatarajiwa kufanyika 19 Julai 2026, kwenye Uwanja wa MetLife huko New Jersey, Marekani.

Ikumbukwe  Infantino, Machi 5, 2025 kupitia ukurasa wake wa Instagram alitoa taarifa ya kuwepo kwa burudani ya muziki katika kipindi cha mapumziko kwenye Fainali za Kombe la Dunia 2026.

“Ninaweza kuthibitisha onyesho la kwanza kabisa la muda wa mapumziko kwenye fainali za kombe la dunia la FIFA, kwa ushirikiano na Global Citizen. Huu utakuwa wakati wa kihistoria kwa Kombe la Dunia,” aliandika Infantino.

Hatua hii ya FIFA kutumia muda wa mapumziko kutoa burudani ya muziki kwenye fainali za Kombe la Dunia 2026 imekuja kufuatia Super Bowl Half Time Show ya mwaka 2025, aliyotumbuiza Kendrick Lamar kuacha alama kubwa kwenye ulimwengu wa burudani huku ikiongeza thamani ya mchezo husika.