
Desemba 29, 2024, yaani siku mbili kabla ya kuingia mwaka 2025, lakini ikiwa imepita miezi miwili na siku 28 tangu alipotimiza umri wa miaka 100, Rais wa 39 wa Marekani, Jimmy Carter, alifariki dunia.
Ni Rais pekee wa Marekani kubaki hai baada ya kuondoka madarakani hadi kutimiza umri wa miaka 100. Pamoja na hivyo, hilo siyo kubwa. Carter ni mada nzito kisiasa Marekani kwa jinsi watu wengi wanavyompa kadirio la chini la ufanisi ofisini kuliko rekodi halisi alizotengeneza.
Sera za Carter kwenye mazingira, elimu na afya, zinampambanua kama kiongozi aliyefanikiwa zaidi kwenye sekta hizo. Kikubwa ni jinsi alivyoweza kufanikisha Mkataba wa Camp David, baina ya Israel na Palestina. Carter aliingia madarakani Januari 20, 1977.
Ndani ya mwaka mmoja na siku 28, alifanikisha mazungumzo ya amani baina ya Palestina na Israel. Ilipofika Septemba 17, 1978, Carter alishiriki kusaini Mkataba wa Camp David.
Upande wa Israel, alisaini aliyekuwa Waziri Mkuu, Menachem Begin, upande wa Palestina, na kwa niaba ya jumuiya ya Waarabu, mkataba huo ulisainiwa na aliyekuwa Rais Misri, Anwar Sadat. Camp David ni mkataba bora wa amani kuwahi kusainiwa kwa ajili ya Mashariki ya Kati. Kawaida, binadamu huwaundia wenzao makadirio ya juu wanaowapenda na kuwashusha wasiowataka.
Carter alipitia hayo. Uongozi wake unaonekana haukufanikiwa, lakini ulipiga hatua nzuri za kimsingi. Waja wenye hulka ya “kuchukulia poa” wenzao, walipomwona Rais Samia Suluhu Hassan anakula kiapo kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, walidhani wangemchezea watakavyo. Ni mwanamke. Kuna watu waliwahi kusema Rais Samia ni house girl, asingeweza kuendesha nchi (Rais Samia mwenyewe kwenye moja ya hotuba zake).
Kuna ambao walinong’ona wakicheka na kugongeana mikono kuwa ambacho Rais Samia alikuwa anakiweza ni kufunga vilemba tu (walimkebehi hadi uvaaji wake). Machi 19, 2025, Rais Samia atatimiza miaka minne tangu aliposhika uongozi wa juu kabisa wa Dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Karata ambazo Rais Samia amekuwa akizicheza kisiasa, zimewaziba mdomo waliomwita ‘house girl’, zimewatuliza waliombeza kwamba anachojua ni kufunga vilemba. Rais Samia ni sawa na mchezaji wa mchezo wa drafti, ambaye kila mwenye kujitokeza kucheza naye, anajipiga kifuani kwa tambo kuwa atamshinda, lakini kete zinapoanza kusukumwa, ndipo hugundua kuwa kete zake ni ngumu kupitiliza.
January Makamba ni kiongozi mzuri, maarifa yake ya kiuongozi ni makubwa na ametoka kwenye familia yenye mzizi wa uongozi. Baba yake, Yusuf Makamba ni Katibu Mkuu wa CCM mstaafu na alishakuwa mkuu wa mkoa kwa zaidi ya miongo miwili na mbunge.
Kila aliyempima Samia kwa kadirio la chini, asingewaza kumweka kando ya Baraza la Mawaziri January bila kusema neno. Alifanya hivyo. Alimteua kuwa Waziri wa Nishati, akamhamishia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Kipindi January akiwa Waziri wa Nishati, ungejiuliza chuki dhidi yake ilitokea wapi? Alisakamwa mno mitandaoni. Jinsi January alivyoandamwa bila Rais Samia kuchukua hatua yoyote, ilichochea maoni kwamba hagusiki. Ni ‘untouchable’, Ilinenwa kwa Kimang’ati.
Wakati Rais Samia aliona ni mwafaka ampumzishe January, alifanya hivyo na alinyamaza.
Kisha, Februari 24, 2025, Rais Samia akiwa Bumbuli, Tanga, akasema: “Mimi ni Mama, nilimfichia chakula January kumwadhibu, sasa namrudisha mwanangu kwa Mama.” Akamwita, akamkumbatia.
Msamaha wa January, unakumbusha jinsi alivyowaweka kando mawaziri, William Lukuvi na Profesa Palamagamba Kabudi. Wakakaa benchi miaka miwili, halafu akawarudisha tena kwenye Baraza la Mawaziri. Sawa pia na Profesa Kitila Mkumbo.
Rais Samia alimfuta kazi Albert Chalamila akiwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, halafu akamrudisha, akamteua Kagera, halafu akamhamishia Dar es Salaam. Ndani ya miaka minne ya urais wake, Rais Samia amebadilisha wakurugenzi wakuu wa Idara ya Usalama wa Taifa wanne. Kutoka Diwani Athumam mpaka Said Massoro, ambaye alipoondolewa aliingia Ali Siwa, halafu kwa sasa Idara ya Usalama wa Taifa (Tiss), inaongozwa na Suleiman Mombo. Kila kitu kinatoa jibu kuwa kete za Rais Samia ni ngumu, na kwamba kwenye drafti lake, yeye ndiye bosi.
Julai Mosi, 2022, Rais Samia alitambulisha falsafa ya R Nne, ambazo aliahidi kuzitumia kuendesha siasa za nchi. Reconciliation (Maridhiano), Resilience (Ustahimilivu na unyumbulifu), Reform (Mabadiliko) na Rebuilding, yaani ujenzi mpya wa nchi. R moja yenye kubeba Maridhiano, imeingia ndani ya Chadema na ACT-Wazalendo. Chadema wametoka kunyukana kwenye uchaguzi mkuu wao ambao kilele chake kilikuwa Januari 21, 2025. Mwenyekiti mpya, Tundu Lissu na mtangulizi wake, Freeman Mbowe, walivurugana kupita kiasi.
Sehemu kubwa ya kampeni za uenyekiti Chadema, ilibebwa na agenda ya Maridhiano. Lissu akimtuhumu Mbowe kukipeleka chama arijojo kupitia Maridhiano na Rais Samia. Kipindi ambacho Chadema wanavurugana na chama kukatika pande mbili, Rais Samia alikuwa kimya.
Kete yake Maridhiano iliichimba Chadema, wakati huo yeye katika Mkutano Mkuu wa CCM, Januari 18 na 19, 2025, lilifanyika tukio la kihistoria kwa kupitishwa kuwa mgombea urais wa CCM, nje ya utaratibu na utamaduni wa chama hicho.
Sasa, kama kulikuwa na mwenye kusudi la kumpa changamoto Rais Samia ndani ya CCM Uchaguzi Mkuu 2025, ameshapoteza kete. Mchezo wa drafti una kete dume ambayo huitwa king. Uongozi wa Rais Samia umethibitisha kuwa drafti lake, kila kete yake ni king.
Inakula kushoto na kulia, mbele na hata nyuma. Inakula kete za mbali na inamega za karibu. Waliosema anaendeshwa hakubishana nao kwa maneno, bali matendo yamempambanua kuwa yeye ndiye bosi. Na hakuna ubishi tena.