DR Congo yaishitaki Rwanda mahakama ya Afrika

Arusha. Mvutano wa kisheria umeibuka katika kesi iliyofunguliwa na Seriakali Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) dhidi ya Rwanda kwenye Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR) iliyopo jijini Arusha.

DRC ilifungua kesi Agosti 2023 na imeanza kusikilizwa leo Februari 12, 2025, mbele ya majaji tisa, ikiongozwa na Rais wa Mahakama hiyo, Jaji Imani Daud Aboud kutoka Tanzania.

Wakati DRC ikiwakilishwa na jopo la mawakili 17 ikidai Rwanda imekuwa ikifanya vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu, Serikali ya Rwanda imejibu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo kwani mambo yanayoendelea DRC ni mapigano na si ukiukwaji wa haki za binadamu.

Pia, Rwanda imedai mahakamani hapo kuwa DRC inajaribu kuleta hoja ambayo haikuwepo mwaka 2023 na kwamba inatumia kesi hiyo kuingiza hoja ya mapigano yanayoendelea sasa mashariki mwa DRC.

Katika kesi hiyo, DRC inadai ukiukwaji wa haki za binadamu ikiwemo utekelezaji wa matukio ya mauaji ya halaiki, vitendo vya udhalilishaji kama vile ubakaji, na maneno ya kashfa.

Pia, DRC inadai Rwanda inafanya uharibifu wa miundombinu ya huduma za kibinadamu kama shule, hospitali, umeme na maji, yote yakitekelezwa na vikundi vya waasi vinavyodhaminiwa na Serikali ya Rwanda.

DRC inasisitiza kuwa Rwanda inatekeleza vitendo hivi ikijua kwamba ni kinyume na haki za binadamu na kwamba inakiuka mikataba ya kimataifa ambayo imeingia nayo.

Jopo hilo la mawakili wa DRC, liliendelea kudai mahakamani hapo kuwa zaidi ya watu milioni mbili wameathiriwa na vitendo hivyo, wakiwamo waliouawa na wengine wakikimbia makazi yao huku wengine wakifa polepole kutokana na magonjwa, njaa, na ukosefu wa huduma za kibinadamu, ikiwemo matibabu.

“Sababu ya yote haya ni tamaa ya Rwanda ya kupora rasilimali za nchi yetu, hasa katika Kivu ya Kaskazini na Kusini, ambapo hata mji wa Goma umeathirika, na wananchi wengi wameuawa na wengine wakikimbia makazi yao,” amesema mmoja wa mawakili hao, Samuel Kabuya, na kuongeza;

“Hadi sasa, tuna ushahidi wa picha unaoonyesha kuwa Rwanda inasaidia makundi ya waasi yenye zaidi ya wanachama 3,000, na hadi Januari 2025, baadhi ya maeneo tayari yamechukuliwa na makundi haya,” amesema.

Ukiukwaji unaodaiwa unahusiana na mzozo wa silaha unaoendelea katika sehemu ya mashariki ya DRC tangu 2021, ambapo majeshi ya DRC yanapigana na kundi la waasi la M23, ambalo linaripotiwa kuungwa mkono na Rwanda.

Hata hivyo, Rwanda iliyowakilishwa na jopo la mawakili nane wakiongozwa na Waziri wa Sheria na pia Wakili Mkuu wa Serikali ya Rwanda, Emmanuel Ugirashebuye, alidai kuwa madai yaliyotolewa na DRC dhidi ya Rwanda si ya kweli, hivyo kuiomba mahakama hiyo kutupilia mbali shauri hilo.

Moja ya sababu aliyodai mahakamani hapo ni kutokana na Rwanda kujiondoa kwenye itifaki inayounda mahakama hiyo, inayotoa ruhusa ya nchi hiyo kushtakiwa au kushtaki watu na mashirika moja kwa moja.

Pia, amedai DRC imechanganya majukumu ya mahakama, ambayo inapaswa kusikiliza mashauri yanayohusu haki za binadamu tu, na si migogoro ya vita inayosababishwa na mambo ya kisiasa.

“Tunaomba mahakama itupilie mbali kesi hii na isikubali kuingizwa kwenye mambo ambayo yako nje ya mamlaka yake, kwani hiyo itavuka mipaka yake ya kijiografia,” amesema na kuongeza;

“Lakini pia tunaomba mahakama ijiridhishe kuhusu kesi hii, kwani wakati mlalamikaji (DRC) anaifungua, hatukuwa na mgogoro nao, hivyo kufanya hivyo kunadhihirisha kuwa wanajaribu kuileta mahakama hii katika mgogoro usiohusika,” amesisitiza.

Aidha, kesi hiyo itaendelea tena kesho, Februari 13, 2025, katika mahakama hiyo, ambapo majaji wataendelea kusikiliza ushahidi na kuamua hatma ya kesi hiyo.