Dr. Almasi aukataa uzee, ajifananisha Snoop Dogg

Dar es Salaam. Kuzeeka ni mpango wa Mungu ila kuchoka ni kujitakia. Kauli hii ameitoa Mwigizaji Steven Charles Almasi ‘Dr. Almasi’

Baada ya  kuzungumza na Mwananchi  Dr. Almasi aliyetambulika kwa kuvaa uhusika katika filamu na Tamthilia mbalimbali ameeleza kuwa licha ya kuwa na familia yenye watoto watatu na wajukuu lakini bado ameendelea kujikubali na kuishi katika mtindo wake mwenyewe.

“Mimi nina watoto na wajukuu lakini sijaruhusu kuchoka bado najikubali kutokana na mtindo wangu wa maisha kwa sababu ukiangalia katika jamii yetu wazee wengi wamejichagulia kuchoka na kuchakaa sasa mimi kwangu ni tofauti sijachagua kuchakaa.

“Walio wengi wanaamini ukiwa mzee au umri umeenda basi hutakiwi kuvaa vizuri, kujipulizia pafyume na kwenda na dunia inavyoenda hususani kwa zama za sasa,” amesema.

Kutokana na mwonekano wake amesema unampatia deal nyingi za mambo ya fashion huku akidai kuwa anawatazama zaidi Snoop Dogg, P Diddy, R Kelly

“Watu wanatakiwa wajue mimi siishi katika mipaka ya Tanzania au life style ya hapa kwa sababu mimi ni fashionist ambaye naangalia mitindo na mionekano kutoka njee hususa kwa wasanii wenye umri kama wa kwangu ambao tumeachana miaka miwili au mitatu kama akina Snoop Dogg, P Diddy, R Kelly” Anasema Dr. Alimasi

Licha ya kuzungumzia mwonekano wake hakuacha  kuelezea namna soko la uigizaji Tanzania linavyoenda kwa kasi kutokana na wakati.

“Sasa hivi soko la ugizaji kwa hapa Tanzania linaenda kwa kasi sana kutokana na utandawazi wa mitandao na ndiyo maana unaona kuna thamthilia nyingi tofauti na zamani ambapo kazi zilikuwa zinawekwa kwenye DVD au mikanda.” Anasema.

Kipi kinamfanya kuwa bora katika ugizaji?

Ubora au pekee wa mwigizaji unatokana na kitu binafsi alichonacho msanii anapowasilisha kazi yake ya sanaa kwa upande wa Almasi amedai kuwa hajawahi kusemwa vibaya katika kazi yake zaidi ya watu kupenda swaga zake na mtindo wa pekeyake katika sanaa.

“Namshukuru Mungu tokea nilipoanza sanaa sijawahi kuzungumziwa vibaya katika kazi zangu zaidi ya kupewa maua yangu siku hadi siku kwa sababu ya watu wanapenda ‘swaga’ zangu namna ninavyocheza katika filamu kama uhalisia wa kweli.

“Wakati nilipokuwa mtoto hii sanaa ninayofanya sasa hivi ilionekana mapema sana sema wazazi wangu walikuwa wananiona kama mtukutu nisiyesikia kumbe mimi ni staa wa baadaye na hatimaye sasa hivi napata kongole nyingi kutoka kwa mashabiki zangu” Anasema.

Hakutamani kuwa msanii 

Dr. Almasi anaturudisha nyuma kuwa hakutamani kuwa msanii hapo awali japo alikuwa anaishi maisha ya kisanii ambapo mwaka 2017 aliomba kuwa kwenye filamu ya ‘A lot of money’ wakati huo alikuwa najishughulisha na masuala ya hoteli tu

“Ni Mungu tu amebariki mpaka nimefikia hapa kwa sababu ingawa nilikuwa naishi maisha ya usanii ila mwanzoni sikutamani kuwa msanii ilipofika mwaka 2017 nikaomba nionekane katika filamu hapo ndiyo safari yangu ya ugizaji ilipoanzia kabla ya hapo nilikuwa najishughulisha na masuala ya hoteli” Anasema mwigizaji huyo.

Dr. Almasi ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 60 amewahi kushiriki katika filamu na tamthilia mbalimbali zikiwemo Dosari, Olema, Toboa Tobo, Nia, Uhuru Una Gharama Zake, Salamu, Chausiku, Sarafu, Bongo Dar es Salaam na nyingine nyingi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *