
Rais wa Marekani amebaini usiku wa Jumapili kuamkia Jumatatu, Machi 17, kwamba atazungumza na mwenzake wa Urusi, Vladimir Putin, siku ya Jumanne kama sehemu ya maelewano kati ya Marekani na Urusi ili kumaliza vita nchini Ukraine.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 2
Matangazo ya kibiashara
“Nitazungumza na Rais Putin siku ya Jumanne,” Donald Trump amewaambia waandishi wa habari ndani ya ndege ya rais, Air Force One, na kuongeza kuwa “kazi kubwa imefanywa.” “Mambo mengi tayari yamejadiliwa na pande zote mbili, Ukraine na Urusi. “Tunazungumza juu ya hili, kuhusu kugawana baadhi ya mali,” ameelezea, akimaanisha “ardhi” na “viwanda umeme.”
“Tunataka kuona kama tunaweza kumaliza vita. Labda tunaweza, labda hatuwezi, lakini nadhani tuna nafasi nzuri,” ameongeza Donald Trump.
Mjumbe maalum wa Marekani Steve Witkoff, ambaye nchi yake inaishinikiza Urusi kukubali kusitisha mapigano na Ukraine, amesema Jumapili kwamba viongozi hao wawili watakuwa na “majadiliano mazuri na chanya wiki hii.”
Moscow, Kyiv na Washington “wanataka mgogoro huo uishe,” mwanadiplomasia huyo amekiambia kituo cha CNN.
Marekani imekuwa ikitaka kusitisha mapigano mara moja na imetoa shinikizo kubwa kwa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, ambaye alikubali kusitishwa kwa mapigano kwa siku 30 siku ya Jumanne ya wiki iliyopita. Lakini Rais wa Urusi Vladimir Putin alizungumza kuhusu “maswala muhimu” ambayo lazima yashughulikiwe kabla ya usitishaji vita wowote kuafikiwa.
Siku ya Ijuma Ikulu ya Kremlin ilisema kwamba Vladimir Putin aliwasilisha ujumbe kwa mjumbe wa Marekani kwa Donald Trump kuhusu pendekezo lake la kusitisha mapigano kwa siku 30, ambalo liliidhinishwa na Ukraine lakini sio Urusi.
Moscow inataka dhamana ya “kudumu” kwa makubaliano yoyote ya amani
Vladimir Putin hadi sasa ameweka masharti ya juu zaidi ya kukomesha mzozo huo, kama vile Ukraine kuachia maeneo matano yaliyotwaliwa na Moscow, kuachana na malengo yake ya kujiunga na NATO, na kuisambaratisha serikali ya Ukraine.
Moscow itahitaji dhamana ya “kudumu” kama sehemu ya makubaliano yoyote ya amani na Kyiv, ikiwa ni pamoja na uhakika kwamba Ukraine haitajiunga na NATO, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Alexander Grushko amesema katika mahojiano na Gazeti la Izvestia yaliyorushwa leo Jumatatu, Machi 17.
“Tutaomba dhamana ya usalama ya kudumu ili kuwa sehemu ya makubaliano yoyote,” alisema, bila kutaja pendekezo la kusitisha mapigano la siku 30 lililotolewa na Marekani na kukubaliwa na Ukraine wiki iliyopita wakati wa mkutano nchini Saudi Arabia kati ya maafisa wa ngazi za juu.
“Mpira uko kwenye uwanja wa Urusi,” Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer alisema, akiongeza kuwa “hivi karibuni au baadaye itabidi kushiriki katika majadiliano mazito” Putin ndiye “aliyejaribu kuchelewesha” mambo.
Kwa muda wa wiki mbili, Keir Starmer na Emmanuel Macron wamekuwa wakitafuta kuunda “muungano wa walio tayari” ambao ungetuma wanajeshi katika ardhi ya Ukraine endapo mapigano yatasitishwa, ili kuizuia Urusi kushambulia tena baadaye, jambo ambalo Moscow haitaki kusikia.
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, ambaye siku zote amekuwa akitetea uadilifu wa ardhi ya Ukraine, alimhakikishia Donald Trump siku ya Jumapili “uungwaji wake mkono” kwa juhudi “za moja kwa moja na madhubuti” za Marekani zinazolenga kumaliza vita.