Rais wa Marekani Donald Trump ameagiza kutumwa kwa wanajeshi 2,000 wa kikosi cha walinzi wa taifa huko Los Angeles Jumamosi, Juni 7, msemaji wake ametangaza, kufuatia makabiliano katika mji wa California wakati wa maandamano ya kupinga kukamatwa kwa wahamiaji haramu.
Imechapishwa:
Dakika 3 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
“Rais Trump ametia saini hati ya kirais inayotaka kutumwa kwa wanajeshi 2,000 wa kikosi cha walinzi wa taifa kushughulikia uvunjaji wa sheria ambao umeendelea kushika kasi,” amesema msemaji wa Ikulu ya White House Karoline Leavitt, akilaumu viongozi ” wasiowajibika” kutoka chama cha Democratic huko California.
Mamlaka za Marekani zinaendelea na operesheni zao dhidi ya wahamiaji, kwa kutumia mbinu zinazozidi kuleta utata. Siku ya Ijumaa, Juni 6, polisi wa uhamiaji walifanya uvamizi katika ngome ya chama cha Democratic, jiji la Los Angeles. Kutokana na upinzani wa waandamanaji, Donald Trump ameamua kupeleka wanajeshi wa kikosi cha walinzi wa taifa huko California. Wakati huo huo, huko New York, maafissa wa uhamiaji waliwakamata wahamiaji wawili siku ya Ijumaa katika jengo la mahakama.

Los Angeles inaweza kujionyesha kama mji mtakatifu, lakini hiyo haizuii kukamatwa kwa wahamiaji. Wiki hii, Polisi ya Uhamiaji iliongeza operesheni zake. Zaidi ya watu 40 walikamatwa, jambo lililozua hasira miongoni mwa waandamanaji. Makabiliano yalizuka katika vitongoji kadhaa.
Idara ya polisi ya Los Angeles inadai kuwa haikushiriki moja kwa moja katika operesheni hiyo, lakini inakiri kuwa iliweza kuwalindia usalama maafisa wa shirikisho dhidi ya waandamanaji. Watu kadhaa walikamatwa kwa kukabiliana na maafisa wa Polisi ya Uhamiaji (ICE).
Maafisa wa ICE walikusanyika Jumamosi asubuhi huko Paramount, kitongoji cha Los Angeles chenye Wahispania wengi, karibu na duka kubwa la vifaa vya Home Depot, ambapo wafanyakazi wanakuja kutoa huduma zao kwa siku. Haijulikani ikiwa maafisa wa ICE walikuwa wakijiandaa kuwakamata wahamiaji haramu au walikusanyika tu hapo kujiandaa kwa operesheni nyingine. Hata hivyo, waandamanaji walianza kukusanyika, na idara ya sheriff ilisema ilipeleka maafisa kwenye eneo la tukio asubuhi sana huku mvutano ukiongezeka. Waandamanaji walirusha vitu kwa vikosi vya usalama na kujaribu kuzuia basi kuondoka kwenye eneo la tukio. Maafisa waliwarudisha nyuma kwa vitoa machozi na maguruneti ya kuwatawanya. Kufikia alasiri, mitaa ilikuwa imejaa uchafu, kulingana na picha za vyombo vya habari vya Marekani, ambavyo pia vimeripoti kwamba waandamanaji walichoma moto bendera ya Marekani.
Kufuatia makabiliano haya, Donald Trump alitangaza kutumwa kwa wanajeshi 2,000 wa kikosi cha walinzi wa taifa huko Los Angeles, kulingana na msemaji wake.
Kwa kutuma wanajeshi hao, Donald Trump anarejelea kauli za kihafidhina zinazoiona California-inayoongozwa na Gavin Newsom, gavana kutoka chama cha Democratic kama eneo lisilo na sheria. Ijapokuwa mfumo wa kisheria ambao Donald Trump anatuma wanajeshi hao haujabainishwa, unaweza kuwa umetokana na Sheria ya Uasi ya karne ya 19, sheria inayoruhusu serikali ya shirikisho kuhamasisha jeshi bila idhini ya gavana. Huu ni ujanja kwa rais kuwa na sauti ya mwisho, anaelezea mwandishi wetu huko Atlanta, Edward Maille.
Hii ni operesheni ya pili kwa kiwango kikubwa huko California katika muda wa chini ya wiki moja, kufuatia uvamizi kwenye mgahawa wa San Diego, ambao ulikatishwa kutokana na uhamasishaji wa raia. Gavana huyo kutoka chama cha Democratic ameshutumu operesheni hiyo na kuiita “ukatili.” Meya wa Los Angeles alizungumza juu ya “ugaidi uliopandikizwa katika jiji hilo.” Ni lazima kusema kwamba mbinu zinazidi kuwa nzito.