Donald Trump atangaza ushuru wa asilimia 25 kwa alumini na chuma zinazoingizwa Marekani

Marekani itatoza asilimia 25 ya ushuru wa forodha kwa alumini na chuma zitakaingiza nchini kuanzia Jumatatu, Februari 10, Rais Donald Trump ametangaza siku ya  Jumapili.

Imechapishwa:

Dakika 2

Matangazo ya kibiashara

Baada ya kuwa tayari kuweka asilimia 10 ya ushuru mpya wa forodha kwa bidhaa zinazotoka China, mkuu wa nchi ameongeza kuwa pia ataweka vikwazo vipya vya forodha siku ya Jumanne, kulingana na habari iliyoripotiwa na kundi la waandishi wa habari walioandamana naye kwenye ndege ya rais.

Rais Donald Trump ametangaza Jumapili kwamba ana mpango wa kutoza ushuru wa asilimia 25 kwa chuma na alumini zinazoingizwa nchini Marekani, kuanzia Jumatatu. Atatangaza “Jumanne au Jumatano” ushuru mwingine wa forodha unaolenga kuanzisha uhusiano wa “kubadilishana” bidhaaa na nchi fulani.

“Nitatangaza ushuru wa chuma siku ya Jumatatu. (…) Vyuma vyote vinavyowasili Marekani vitatozwa ushuru wa 25%,” ametangaza mkuu wa nchi kwenye ndege ya rais iliyokuwa ikimpeleka New Orleans kuhudhuria Super Bowl, fainali ya ligi ya soka ya kulipwa nchini Marekani.

Bilionea huyo wa chama cha Republican ameongeza kuwa hata hiyo  itachukuliwa kwa alumini iliyoagizwa kutoka nje.

Wakati wa muhula wake wa kwanza (2017-21), Donald Trump alitoza ushuru wa forodha kwa chuma na alumini ili kulinda tasnia ya Marekani ambayo aliona kuwa inakabiliwa na ushindani usio wa haki kutoka kwa nchi za Asia na Ulaya.

Donald Trump pia amebaini kwamba atatangaza “ushuru wa forodha” “Jumanne au Jumatano” ili kuoanisha ushuru wa bidhaa zinazoingia Marekani na jinsi bidhaa za Marekani zinavyotozwa ushuru nje ya nchi.

“Wakitutoza ushuru wa asilimia 130 na sisi tukaacha hivo, tusiwatoze kodi, haitakaa hivyo,” amesema. “Haitaathiri nchi zote kwa sababu baadhi zina ushuru sawa na sisi. Lakini wale ambao watataka kunufaika kupitia Marekani watachukuliwa hatua.”

Ushuru, ngao ya sera ya kiuchumi ya Trump

Tangu kuapishwa kwa Donald Trump mwezi Januari, ushuru wa forodha umekuwa kiini cha sera yake ya kiuchumi na kidiplomasia, inayoonekana kama njia ya kupunguza nakisi ya biashara ya Marekani kama vile chachu ya mazungumzo na nchi zinazolengwa.

Tangu Jumanne, bidhaa kutoka China zimefanywa kuwa ghali zaidi kwa ushuru wa forodha wa 10% – hatua ambayo Beijing imeamua kulipiza kisasi kwa malipo yaliyolengwa kwa baadhi ya bidhaa za Marekani kuanzia Februari 10.

Ushuru mpya wa China unaathiri bidhaa za Marekani zenye thamani ya dola bilioni 14, huku ushuru uliotangazwa na Donald Trump ukiathiri bidhaa za China zenye thamani ya dola bilioni 525.

Mauzo ya nje kutoka Mexico na Canada hadi Marekani pia awali yalikabiliwa na ushuru (wa 25%) licha ya makubaliano ya biashara huria kati ya nchi tatu za Amerika Kaskazini. Lakini Donald Trump, ambaye anawashutumu majirani zake wawili kwa kutofanya vya kutosha kuzuia ulanguzi wa dawa za kulevya, aliwapa ahueni ya mwezi mmoja katika dakika ya mwisho baada ya kupokea ahadi za kuimarisha usalama wa mpaka.

Katika mahojiano yaliyotangazwa Jumapili na kituo cha Marekani cha CNN, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ametangaza kwamba Wazungu lazima “wawe tayari (…) kukabiliana” na vikwazo vipya vya forodha.

Emmanuel Macron pia ameonya juu ya athari ya hatua hiyo kwa Wamarekani: “Ikiwa utatoza ushuru wa forodha kwa sekta kadhaa, hii itasababisha kuongezeka kwa bei na kusababisha mfumuko wa bei nchini Marekani.”