Dodoma yabainika kuwa ukanda wa madini mengi

Dodoma. Taasisi ya Utafiti na Madini Tanzania (GST) imesema changamoto inayowakabili wachimbaji wadogo nchini ni ukosefu wa elimu ya uchenjuaji madini wanayoyachimba na kuwataka wawasiliane na GST ili waelekezwe namna ya kuchenjua madini hayo kwa tija.

Taasisi hiyo pia imesema kuwa wachimbaji hao hawana elimu ya kutosha ya kujua teknolojia mbalimbali za uchenjuaji wa madini na hivyo hujikuta wakipoteza thamani ya madini hayo kwa kutumia kemikali ambazo hazihusiki na uchenjuaji wa madini husika.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Machi 27, 2025 jijini Dodoma, Kaimu Mtendaji Mkuu wa GST, Notka Banteze amesema ili kujenga uelewa wa ramani yanapopatikana madini nchini, GST imetoa kitabu kinachoonyesha ramani ya maeneo hatari kwa matetemeko ya ardhi, maporomoko ya udongo huku Mkoa wa Dodoma ukiongoza kwa kuwa na aina nyingi za madini tofauti tofauti.

Amesema wachimbaji hao pia hawana elimu ya kutambua mlalo wa miamba, kina cha miamba na uchenjuaji wa miamba hiyo ili wapate ugunduzi mkubwa.

“Sisi kwa wachimbaji wadogo tumejikita zaidi kwenye upande wa utoaji wa elimu, na elimu hii inawasaidia namna ya kutambua miamba, wakishatambua ile miamba uchukuaji wa sampuli uwakilishi uweje ili hata anapopeleka maabara sampuli ile apate majibu ambayo yanakuwa wakilishi na yanamaanisha kile ambacho anaendelea nacho,” amesema.

Amesema wamejitahidi kuwafikia wachimbaji wadogo ambapo wameongeza wigo wa kutoa ushauri elekezi kwa wachimbaji hao ili kuwatia moyo na kuwavutia waitumie GST kupata ushauri wa kitaalamu utakaowawezesha kuchimba kwa tija zaidi.

“Kitu kingine ambacho tuliona kinaleta shida kwa wachimbaji wadogo ni uchenjuaji, katika eneo la uchenjuaji kuna shida kubwa moja kujua sifa za miamba, ukishajua sifa za miamba maana yake kuna utaratibu wa kisayansi ambao unatakiwa kutumika kuichenjua ile miamba na sehemu kubwa ya nchi yetu imekuwa ni changamoto sana kwa wachimbaji wadogo,” amesema Banteze.

Amewataka wachimbaji wachukue sampuli zao wazipeleke GST ambako kuna maabara za uchenjuaji ambao watafanya tafiti zao za ndani kupitia sampuli hiyo na tafiti hizo zitawapa uwiano mzuri wa kemikali ili wawashauri wanapokwenda kuchenjua wachenjue kwa tija.

Ametaja aina za madini zinazopatikana nchini kuwa ni madini ya metali, madini ya nishati,  madini ya viwanda, madini mkakati na madini adimu ambapo mkoa wa Dodoma ndiyo unaoongoza kwa kuwa na madini mengi ya aina tofauti tofauti.

Amesema mkoa wa Dodoma uko kwenye ukanda maalum wa jiolojia unaupitiwa na mabadiliko tofauti ya kijiolojia na kuufanya kuwa na orodha ya madini mengi ya aina mbalimbali kuliko mikoa mingine.

Amesema baadhi ya madini hayo ni madini mkatakati kama vile Lithium, Nikel, Chuma, Urani, Shaba na Helium. Madini mengine ni kwa ajili ya matumizi ya viwanda vya ndani ambayo ni Chokaa, Jasi, Feldspar, Mfinyanzi, Quartz na Kyanite.

Madini mengine ambayo ni ya kipekee kwa sasa yanayopatikana Tanzania tu ambayo ni madini ya Yoderite ambayo yako katika Mlima wa Mautia Wilaya ya Kongwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *