Dodoma, Pwani mikoa vinara kwa umaskini lakini muhimu kwa uchumi

Dar es Salaam. Ingawa Mkoa wa Dodoma ndio makao makuu ya nchi, wakazi wake bado wanahesabika kuwa miongoni mwa watu maskini zaidi nchini, takwimu zinaonyesha.

Vivyo hivyo, kwa Mkoa wa Pwani, ambao ukaribu wake na Dar es Salaam na kukua kwa kasi kwa sekta ya viwanda, hakukuwasaidia wakazi wake kuinuka kiuchumi, kwani takwimu zinaonesha nao ni maskini.

Hayo ni kwa mujibu wa Ripoti Jumuishi ya Utendaji wa Kiuchumi wa Kanda kwa Septemba 2024, iliyochapishwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).

Ripoti hiyo, inaonesha Dodoma ni miongoni mwa mikoa mitano yenye kiwango kidogo cha pato la mtu mmoja, ukilinganisha na mingine nchini.

Kulingana na ripoti hiyo ya Machi 7, 2025, pato la wastani la mtu mmoja mkoani Dodoma lilikuwa Sh1.901 milioni hadi kufikia Septemba 2024, huku Mkoa wa Pwani ukiwa na pato la Sh1.831 milioni kwa mwaka 2023.

Mikoa mingine yenye pato dogo zaidi ni Singida (Sh1.711 milioni), Kagera (Sh1.559 milioni) na Simiyu (Sh1.552 milioni).

Kwa upande mwingine, Dar es Salaam inaongoza kwa pato la juu zaidi la mtu mmoja, likifikia Sh5.743 milioni mwaka 2023.

Kinachoshangaza Iringa, mkoa unaotegemea kilimo unashika nafasi ya pili kwa pato la juu la mtu mmoja, likifikia Sh4.816 milioni, huku pato lake la jumla kwa bei za sasa likiwa Sh5.942 trilioni. Mazao makuu yanayolimwa mkoani humo ni alizeti, nyanya na chai.

Mbeya inashika nafasi ya tatu kwa pato la Sh4.361 milioni kwa mtu mmoja, ikichochewa na shughuli za kilimo, uchakataji wa mazao, viwanda na madini.

Ruvuma, inayojulikana kwa uzalishaji wa chakula, uvuvi katika Ziwa Nyasa, ukataji mbao na ufugaji nyuki, inashika nafasi ya nne kwa pato la Sh3.677 milioni kwa mtu mmoja.

Mkoa wa Kilimanjaro, unaoendelea kwa kilimo, viwanda na utalii, unashika nafasi ya tano kwa pato la Sh4.344 milioni kwa mtu mmoja.

Njombe, inayojulikana kwa uzalishaji wa viazi mviringo, mahindi, maharage, mbao na nguzo za umeme, inashika nafasi ya sita kwa pato la Sh3.705 milioni kwa mwaka 2023.

Arusha, mkoa unaoongoza kwa utalii, unashika nafasi ya saba kwa pato la Sh3.667 milioni kwa mtu mmoja, sambamba na Mwanza ambayo inategemea kilimo, uvuvi na madini, ikiwa na pato la Sh3.555 milioni.

Mikoa mingine katika orodha ya mikoa kumi bora kwa pato la juu la mtu mmoja ni Manyara (Sh3.311 milioni), Tanga (Sh3.255 milioni) na Mtwara (Sh3.039 milioni).

Kwa nini Dodoma, Pwani

Akizungumza na gazeti hili, Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Lutengano Mwinuka alisema tatizo kuu katika Mkoa wa Pwani ni kutoendelezwa ipasavyo kwa rasilimali za bahari.

“Mkoa huu unategemea sana uchumi wa baharini kwa ustawi wa wananchi wake, lakini bado haujatumiwa kikamilifu,” alisema Dk Mwinuka.

Aliongeza bado kuna matumizi ya mbinu duni za uvuvi, huku fursa kama ufugaji samaki wa vizimba na uchakataji wa mazao ya baharini hazijapewa msukumo wa kutosha.

Kwa upande wa Dodoma, Dk Mwinuka alieleza ongezeko la watu halijalingana na ukuaji wa uzalishaji wa kilimo, hivyo kusababisha kudorora kwa kipato cha wakazi wake.

“Hakuna juhudi kubwa za kutafuta masoko mapya kwa ajili ya mazao ya wakulima, jambo linalosababisha wananchi kuteseka wanapokabiliwa na ongezeko la bei ya bidhaa, kwani kipato chao kinasalia vilevile,” alisema.

Mwanazuoni mwingine wa uchumi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk Daidi Ndaki alisema hali ya kiuchumi ya Dodoma ilitarajiwa kutokana na ongezeko la mahitaji ya ardhi.

“Katika miaka ya hivi karibuni, ongezeko la mahitaji ya ardhi limeingizia halmashauri mapato makubwa. Hata hivyo, chanzo hiki cha mapato si endelevu kwa kuwa ardhi ni rasilimali isiyoongezeka, hivyo biashara ya mauzo ya ardhi haiwezi kudumu milele,” alieleza.

Kwa upande wa Pwani, Dk Ndaki alisema licha ya uwekezaji mkubwa kwenye miundombinu, ukuaji wa pato la Taifa bado upo chini.

“Pwani ilishuhudia ongezeko la mapato ya muda mfupi wakati wa maendeleo ya viwanda kutokana na mauzo ya ardhi, kama ilivyo kwa Dodoma. Lakini mapato haya si endelevu,” alisema.

Dk Ndaki alishauri Serikali ianzishe mfumo wa mgao wa mapato kati ya kanda ili kusaidia mikoa iliyo nyuma kiuchumi.

“Kwa mfano, Mkoa wa Pwani huzalisha bidhaa nyingi zinazouzwa Dar es Salaam. Ikiwa kutakuwepo na makubaliano rasmi, mikoa yote miwili inaweza kufaidika na mapato yatokanayo na bidhaa hizi,” alipendekeza.

Matokeo ya ripoti hiyo yanaonyesha tofauti kubwa ya kiuchumi kati ya mikoa ya Tanzania, hali inayoibua haja ya sera maalumu za kiuchumi ili kuinua mikoa kama Dodoma na Pwani, licha ya umuhimu wao kwa maendeleo ya Taifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *