Dk Nyambura afunguka mapito ya mwanamke katika uongozi

Dar es Salaam. Miongoni mwa wanawake wanasayansi ambao wamefanikiwa kiuongozi kwa Tanzania, hutosita kumtaja Dk Nyambura Moremi, Mkurugenzi wa Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii.

Nyambura ambaye ni mtaalamu wa maikrobaolojia, anayeongoza nafasi hiyo kwa mara ya pili, amefanya mahojiano maalumu na  Mwananchi, kuhusu uongozi, nafasi yake katika jamii na jinsi alivyopambana na mlipuko wa Uviko-19 mwaka 2020.

Nafasi ya uongozi

Akizungumza kuhusu nafasi yake ya uongozi katika taasisi hiyo, anasema hakuna changamoto kubwa iliyomfanya ashindwe kutekeleza majukumu yake kwa sababu ya jinsi aliyonayo.

Dk Nyambura anasema amefanya kazi sehemu mbalimbali kabla ya kuifikia nafasi hiyo.

Anasema mara nyingi, mwanamke kiongozi anapochukua mtazamo wa upole na kuendesha mambo kwa utaratibu, huonekana kama uongozi wake unalegalega au hana uthabiti wa kufanya uamuzi.

Anasema hali hiyo imewalazimu wanawake kutumia nguvu kubwa kuonyesha kwamba, wanaweza kuongoza ipasavyo.

Ulinganifu majukumu ya nyumbani, kazini

Akiwa mke na mama wa watoto wawili, Dk Nyambura anataja changamoto nyingine kwa wanawake viongozi kuwa ni ulinganifu kati ya majukumu ya kazi na familia.

“Kuna majukumu ya nyumbani, familia, ndugu na jamaa. Mimi nina watoto bado wadogo, mama asipoonekana kwa wiki mbili, watoto hulalamika, lakini baba akipotea muda huohuo, mara nyingi watoto hawajali,”anasema Dk Nyambura.

Anaeleza jinsi hali hiyo inavyokuwa changamoto kihisia kwa wanawake, hasa wanapohitajika kuondoka kwa muda mrefu.

“Unapokuwa unaondoka, watoto wanalia, hii kihisia ni changamoto kwako. Wakati mwingine umechoka lakini kazi zinakufuata, inabidi uzitekeleze. Wapo wanaokuangalia kama mwanamke, lakini bado unapaswa kupambana kuthibitisha kwamba, dhana potofu zilizopo si sahihi,”anasema Dk Nyambura.

Kuhusu nafasi ya wanawake katika sayansi, Dk Nyambura anasema kuna maendeleo makubwa katika kipindi kifupi na wanawake wengi sasa wanafanya kazi kubwa katika taaluma hiyo.

Anatoa mifano ya wataalamu wanawake akiwamo Dk Zaituni Bokhari, bingwa wa upasuaji wa watoto katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, pamoja na mabingwa wa dawa za usingizi na upasuaji wa mishipa ya fahamu.

Pia, anamtaja Rais Samia Suluhu Hassan, kama kielelezo cha uongozi wa mwanamke, akisema ameonyesha juhudi kubwa kwa kuteua wanawake wenye sifa na kuwawezesha kushika nafasi za uongozi.

“Wanawake wengi wenye uwezo mzuri bado wako katika ngazi za kati na chini, lakini katika uongozi wa juu bado hatujafikia asilimia 30 ifikapo mwishoni mwa mwaka 2023,” anasema.

Hata hivyo, Dk Nyambura anasema amebaini bado kuna jitihada zinaendelea kufanyika kuelekea lengo la usawa wa kijinsia.

Dk Nyambura  anasema kwa sasa watoto wa kike wamewezeshwa zaidi katika masomo ya sayansi, hesabu na uhandisi kupitia mipango kama Samia Scholarship, ambayo imeweka kipaumbele kwa wasichana.

Pia, anasema kuna nafasi za mafunzo ya uongozi ambayo yeye alipata fursa kupitia Uongozi Institute.

Dk Nyambura anasisitiza licha ya uwezeshwa, wanawake wanapaswa kuwa na mwamko wa kuzitafuta fursa za uongozi, akitoa mfano wa mafunzo aliyohudhuria, kati ya waombaji 500, walichaguliwa 50 pekee.

Anawashauri wasichana wanaosoma sayansi, kusoma kwa bidii na kujifunza kutoka kwa waliotangulia.

“Tanzania tuna mifano mizuri; tuna Amiri Jeshi Mkuu mwanamke na vitengo vingi vinaongozwa na wanawake, ikiwamo Maabara ya Taifa. Hakuna njia fupi, kanuni ni zilezile; bidii, nidhamu, na kujifunza kutoka kwa wengine,” anasema Dk Nyambura.

Anaeleza shauku ya kurudi Shule ya Jangwani aliyosoma kuwaonesha wanafunzi wa sasa kuwa, yeye pia alikuwa sehemu ya darasa lao.

“Nilisoma Jangwani na natamani siku moja nirudi pale kuwaonesha wanafunzi kuwa nilikaa hapa. Hii itawatia moyo na kuwaonesha kuwa wanaweza kufanikisha ndoto zao.”

Mwanamke huyo msomi anasema juhudi na bidii pekee hazikumfikisha alipo, bali pia msukumo mkubwa kutoka kwa baba yake, mzee Moremi, aliyemsisitiza kuendelea mbele.

“Nilipohamasika kuwa daktari, baba yangu alikuwa na mchango mkubwa sana katika kunisukuma. Kuna nyakati unapokutana na vikwazo, lakini ukiwa na mtu wa kukutia moyo na kukuambia uendelee, unapata nguvu ya kusonga mbele. Nilijitahidi kufikia lengo langu, nikapambana na hatimaye nikavuka matarajio yangu,” anasema daktari huyo.

Akiwa kiongozi, Dk Nyambura anasema amejifunza kuwa wapo wanawake waliofikia malengo lakini hujirudisha wenyewe nyuma kwa hofu au kutojiamini. Hata hivyo, alipowapa nafasi, wameonyesha uwezo wa hali ya juu.

“Wanawake viongozi wanapaswa kuwavuta wale wanaokaa nyuma. Ukimvuta mmoja tu na kumwamini, unaweza kugundua kuwa alihitaji mtu wa kumuonesha tu kuwa anaweza,” anasema Dk Nyambura.

Maabara ya Taifa

Dk Nyambura anaelezea umuhimu wa Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii, inayotambua milipuko ya magonjwa, kuchambua sampuli na kusaidia kudhibiti magonjwa hayo.

“Maabara hii ina jukumu la kuhakikisha ubora wa vipimo vinavyotumika katika maabara nyingine nchini. Tunapogundua mlipuko mahali fulani, tunatoa mwongozo wa hatua za kuchukuliwa ili kudhibiti maambukizi. Pia, tunafanya tathmini ya mara kwa mara kuhakikisha vipimo vina ubora unaostahili. Vipimo vinavyokosa ubora hufungiwa na mamlaka husika kwa ajili ya usalama wa jamii,” anafafanua Dk Nyambura.

Akizungumzia mafanikio ya maabara hiyo, Dk Nyambura anasema imejenga uwezo wa kubaini vimelea kwa undani zaidi kwa kutumia teknolojia ya vinasaba.

“Kwa sasa tunaweza kutambua aina ya kimelea, chanzo chake, jinsi kinavyosambaa na uhusiano wake na virusi vingine duniani. Hii ni hatua kubwa katika sayansi ya maabara. Tumepiga hatua kiasi kwamba Maabara ya Taifa sasa ni kituo cha umahiri barani Afrika. CDC ya Afrika Mashariki imetutambua kama kituo cha ulinzi na usalama wa vimelea, mataifa kama Ethiopia na Comoro huja kupata mafunzo hapa,” anasema.

Pia, anabainisha kuwa maabara hiyo imepata ithibati ya kimataifa baada ya ukaguzi uliofanyika wiki tatu zilizopita. “Hili ni moja ya mafanikio makubwa niliyoyapata kama kiongozi wa maabara hii,” anasema Dk Nyambura.

Kupambana na milipuko ya magonjwa

Dk Nyambura anasema mlipuko wa Uviko-19 ulikuwa mtihani mkubwa kwa sekta ya afya duniani, lakini pia ulitoa fursa ya kujifunza na kuboresha mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa ya mlipuko.

“Tulijifunza jinsi ya kutambua ugonjwa mapema ili kuzuia usisambae. Tulianzisha mfumo wa tathmini maeneo hatarishi, kuimarisha mafunzo kwa wataalamu wa maabara na kuweka vifaa vya kupima joto katika mipaka na viwanja vya ndege. Mtu yeyote anayeonekana kuwa na dalili za ugonjwa huchukuliwa sampuli kwa uchunguzi wa haraka,” anasema Dk Nyambura.

Anabainisha kuwa, matokeo ya vipimo kutoka Maabara ya Taifa ndiyo huamua iwapo ugonjwa fulani upo nchini au umedhibitiwa.

Changamoto za Uviko-19

Kuhusu changamoto zilizokumba Maabara ya Taifa wakati wa mlipuko wa Uviko-19, Dk Nyambura anakiri kuwa kazi ilikuwa ngumu kutokana na wingi wa sampuli na uhaba wa rasilimali watu.

“Uviko-19 ulisambaa kwa kasi kwa sababu uliambukizwa kwa njia ya hewa. Serikali ilichukua hatua haraka kwa kuongeza mashine na wataalamu. Maabara ilifanya kazi saa 24, lakini kutokana na uhaba wa watumishi, baadhi walilazimika kufanya kazi kwa muda mrefu zaidi ya kawaida. Serikali iliongeza nguvu kazi na hatimaye tukaweza kudhibiti hali hiyo,” anasema Dk Nyambura.

Umuhimu wa chanjo

Dk Nyambura anasema chanjo ilikuwa miongoni mwa suluhisho lililosaidia kudhibiti Uviko-19.

“Tulichanja watu wengi, hiyo ilisaidia kujenga kinga ya jamii. Kirusi kilipoteza makali yake kwa sababu kingamwili zilikuwa tayari zimelipambana nalo,” anasema.

Akitolea ufafanuzi kuhusu chanjo, anasema hufanya kazi kwa kuufundisha mwili jinsi ya kupambana na vimelea vya magonjwa kabla ya maambukizi halisi kutokea.

“Chanjo ni kama mafunzo kwa mwili. Inapowekwa mwilini, inamfundisha jinsi ya kupambana na virusi au bakteria fulani. Kwa hiyo, ugonjwa halisi ukija, mwili tayari una kingamwili za kuupambana,” anasema.

Kuhusu hofu ya watu kwamba chanjo za Uviko-19 zilitengenezwa kwa muda mfupi, Dk Nyambura anasema:

“Ilikuwa dharura, lakini ufuatiliaji wa kisayansi ulifanyika kwa kina. Chanjo hupitia hatua kadhaa kabla ya kuidhinishwa na hapa Tanzania, kuna kamati maalumu ya kitaifa inayohakikisha chanjo yoyote inayotumika imekidhi viwango vya usalama.”

Dk Nyambura anasema juhudi za kisayansi zinaendelea ili kuhakikisha jamii inalindwa dhidi ya milipuko ya magonjwa na Maabara ya Taifa itaendelea kuboresha mifumo yake kwa manufaa ya afya ya umma.