Dk Ndugulile akumbukwa WHO ikifanya uchaguzi

Dar es Salaam. Bodi ya Utendaji ya Shirika la Afya Duniani (WHO) na Kamati ya Kanda ya Afrika, imemkumbuka Dk Faustine Ndugulile na kutuma salamu za rambirambi kwa familia na nchi ya Tanzania kwa kumpoteza kiongozi huyo.

Hayo yamesemwa leo Jumapili, Mei 18, 2025 wakati wa kikao maalumu cha ana kwa ana cha kamati na bodi hiyo ya utendaji kinachofanyika huko Geneva kwa ajili ya kuteua Mkurugenzi wa Kanda ajaye.

Dk Ndugulile alifariki dunia Novemba 27, 2024 wakati akipatiwa matibabu nchini India, alishinda nafasi ya Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika Agosti 27, 2024 katika kikao maalumu cha Kamati ya Kanda ya Afrika kilichofanyika Brazzavile nchini Congo.

Akizungumza wakati wa kufungua kikao hicho leo Kaimu Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika, Chikwe Ihekweazu ameanza kwa kumwelezea Dk Ndugulile kabla ya kuzungumza masuala mengine muhimu.

“Dk Faustiune Ndugulile, alifariki ghafla na kutupatia mshtuko mkubwa sana sote kwa pamoja, alikuwa na maono makubwa na alipanga kuliongoza bara letu kwa vipaumbele muhimu na tulivyovihitaji,” amesema.

Chikwe amemwelezea Dk Ndugulile kama mtu aliyelingana naye umri akisema, “Alikuwa na umri kama nilionao mimi hivi sasa, lakini jukumu letu ni kuendeleza yale yote yaliyokuwa maono yake.”

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk Tedros Ghebreyesus ametoa pole kwa familia, Serikali na Tanzania kwa ujumla kwa kumpoteza kiongozi huyo muhimu.

“Natoa pole nyingi sana kwa familia ya Dk Ndugulile na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali kwa ujumla ni hasara kubwa sana, namshukuru Dk Chikwe kwa kukaimu nafasi hii kwa kipindi chote na kama nilivyosema mwanzo uongozi wako umekuwa mzuri na wa kupigiwa mfano,” amesema Dk Tedros.

Dk Chikwe ameelezea namna ambavyo aliingia katika nafasi hiyo na alivyopata ushirikiano kutoka kwa mataifa mbalimbali barani Afrika.

Amesema tangu alipoanza kutumikia wadhifa huo Februari mwaka huu ilikuwa nafasi nzuri kwake huku akimshukuru Dk Moeti (Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika aliyepita).

“Ninashukuru kwa uongozi wa Moeti kwa kipindi cha miaka 10, amefanya mengi na kutekeleza mengi ambayo tuliyatarajia na ameleta mageuzi makubwa.

“Tangu Februari nilianza kushika nafasi hii kama Mkurugenzi wa WHO Afrika nashukuru ilikuwa ni nafasi nzuri sana ya kufanya kazi nanyi na nimeshukuru kuwa na timu shupavu kabisa,” amesema Dk Chikwe.

Baada ya kifo cha Dk Ndugulile, uchaguzi ulitangazwa kurudiwa tena na Tanzania ilimpendekeza mwanasayansi na mtafiti Profesa Mohammed Janabi kugombea nafasi hiyo, uteuzi uliotangazwa na Rais Samia Suluhu Hassan, akieleza kuwa uzoefu wake katika sekta ya afya unamfanya kuwa mgombea mwenye sifa stahiki kwa nafasi hiyo muhimu kimataifa.

Baada ya majina ya wagombea wa awamu ya pili kupelekwa WHO, majina yalichakatwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus.

Machi 14 mwaka huu Profesa Janabi alitangazwa rasmi kuwa mmoja wa wagombea wanne kwa nafasi hiyo kupitia ukurasa wa mtandao wa Shirika la Afya Duniani (WHO).

Janabi ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), leo anachuana na wagombea wengine watatu kuwania nafasi hiyo.

Orodha ya wagombea mbali na Tanzania ni Dk N’da Konan Michel Yao kutoka Ivory Coast, Dk Dramé Mohammed Lamine kutoka Guinea, na Profesa Mijiyawa Moustafa kutoka Togo.

Mkurugenzi wa kanda huteuliwa na bodi ya utendaji ya WHO baada ya kuteuliwa na kamati ya kanda ya WHO ya Afrika. Uteuzi wa mkurugenzi wa kanda utakuwa kwa kipindi cha miaka mitano, na anaweza kuteuliwa tena mara moja tu.

Nchi yoyote mwanachama wa kanda inaweza kupendekeza mgombea wa wadhifa wa mkurugenzi wa kanda. Mkurugenzi wa Kanda huchaguliwa kwa kura ya siri katika kikao cha faragha cha kamati ya kanda.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *