
Dar es Salaam. Mbunge wa Kigamboni, Dk Faustine Ndugulile amefariki dunia usiku wa kuamkia leo Novemba 27, 2024 nchini India alikokuwa akipatiwa matibabu.
Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson ameeleza hayo katika taarifa iliyotolewa leo Novemba 27.
“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Mbunge wa Kigamboni na Mkurugenzi Mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Kanda ya Afrika, Dk Faustine Ndugulile. Kwa niaba ya wabunge natoa pole kwa familia, wakazi wa Kigamboni na Watanzania wote. Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi,” amesema Spika Tulia katika taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano na Elimu kwa Umma, Ofisi ya Bunge.
Amesema ofisi ya Bunge kwa kushirikiana na familia inaendelea kuratibu shughuli za mazishi na taarifa zaidi zitaendelela kutolewa.
Alitarajiwa kuanza kazi rasmi WHO Machi 2025, baada ya kupewa miezi sita ya kujipanga.
Dk Ndugulile akizungumza Septemba 3, 2024 wakati akitoa shukurani bungeni jijini Dodoma, baada ya kukaribishwa na Naibu Spika wa Bunge, Mussa Zungu alisema:
“Nimepewa miezi sita kujipanga na kuandaa maono yangu nitakapoanza kazi Machi mwakani, nia ya kufanya hivyo ninayo, sababu za kufanya hivyo ninazo na uwezo wa kufanya hivyo ninao.
“Niwaombe mniombee, tuendeleze sala na dua nyingi kwani nafasi hii imebeba maono ya Watanzania na Waafrika wanatarajia makubwa. Kikubwa niishukuru Serikali nzima na wabunge kwa kuniunga mkono, nitakuwepo katika kipindi cha mpito napokea maoni na ushauri kutoka kwenu.”
Dk Ndugulile alikuwa Mtanzania wa kwanza, pia wa kwanza kutoka Afrika Mashariki kushika nafasi hiyo.
Alisema amepewa kipindi cha miaka mitano kuonyesha utendaji wake na iwapo atafanikiwa kufanya vizuri, anaweza kuchaguliwa tena kwa miaka mingine mitano.
“Kituo changu cha kazi kitakuwa Congo Brazzaville, utaratibu ulivyo unapewa miezi sita ya kujipanga hivyo natarajia kuanza kazi mwishoni mwa Februari au Machi 2025.
“Wale waliokuwa wanahoji Jimbo la Kigamboni lipo wazi jibu ni hapana! Bado niponipo na wananchi wangu wote waliniunga mkono na walikuwa na dua zao pia,” alisema.
Dk Ndugulile, mbunge kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) alishinda nafasi ya Mkurugenzi wa WHO, Kanda ya Afrika akiwashinda wagombea wengine ambao ni Dk Boureima Hama Sambo wa Niger, Dk N’da Konan Michel Yao (Ivory Coast), Dk Ibrahima Soc’e Fall (Senegal) na Dk Richard Mihigo (Rwanda).
Dk Ndugulile alipata ushindi huo Jumanne Agosti 27, 2024 baada ya nchi 19 kuipigia kura Tanzania katika mzunguko wa kwanza, 12 wakiipigia Senegal, saba Niger na nchi saba zikiipigia Rwanda.
Matokeo ya ushindi wake yalitangazwa usiku wa Agosti 27, 2024 katika Mkutano wa Afya wa 74 wa WHO uliofanyika Congo Brazzaville.
Katika mzunguko wa pili wa uchaguzi, Dk Ndugulile alipata kura 25, Senegal 14 na Niger kura sita. Dk Ndugulile alipigiwa kura na mawaziri wa afya kutoka Kanda ya Afrika.
Machi 11, 2023, Dk Ndugulile aliteuliwa kuwa mjumbe wa Kamati ya Ushauri Masuala ya Afya ya Umoja wa Mabunge duniani (IPU). Kwa uteuzi huo, alikuwa sehemu ya wabunge 12 duniani wanaoishauri IPU kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu afya.
Uteuzi huo ulianza Februari mwaka 2023 ambao utadumu kwa miaka minne.
Oktoba 24, 2023 Dk Ndugulile alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa kamati ya ushauri ya masuala ya afya ya Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) katika uchaguzi uliofanyika jijini Luanda, nchini Angola.
Kamati ya ushauri ya masuala ya afya ina majukumu ya kushauri mabunge ya nchi na umoja wa mabunge duniani kuhusu masuala yanayohusu afya.
Dk Ndugulile ambaye ni mwanateknolojia, mtungasera, mwanasiasa na mwakilishi wa wananchi wa Kigamboni alizaliwa mwaka
Dk Ndugulile ni nani?
Dk Ndugulile ni daktari mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 25 kwenye afya ya jamii ndani na nje ya nchi.
Amewahi kuwa mwakilishi wa Bara la Afrika katika Taasisi ya kimataifa ya Ukimwi na mwanzilishi wa mtandao wa dunia kuhusu ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB).
Pia, amewahi kuwa Naibu Waziri wa Afya na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari nchini Tanzania.
Machi 11, 2023, aliteuliwa kuwa mjumbe wa kamati ya ushauri masuala ya afya ya Umoja wa Mabunge duniani (IPU).
Oktoba 24, 2023 Dk Ndugulile achaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa kamati ya ushauri ya masuala ya afya ya Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) katika uchaguzi uliofanyika Luanda nchini Angola.