Dk Nchimbi awataka waimbaji wa Injili kuwakumbusha wanasiasa kuomba msamaha

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi ametoa wito kwa wasanii wa Injili nchini kuwakumbusha wanasiasa wasijisahau katika matendo yao na waombe  msamaha wakikosea hususani kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.

Dk Nchimbi amesema wanasiasa wapokuwa wamesimama kwenye kipaza sauti huwa wanajisahau, hivyo hujutia baada ya kwenda kukaa kwenye viti kama wameongea vitu vibaya.

Hayo amesema usiku wa jana Jumapili Aprili 20, 2025 kwenye tamasha la Mtoko wa Pasaka lililofanyika ukumbi wa Super Dome, Masaki, jijini Dar ea Salaam.

Tamasha hilo ambalo hufanyika kila mwaka, linasimamiwa na muimbaji wa injili, Christina Shusho.

Tamasha hilo huzikutanisha kwaya mbalimbali na kusherehekea kufufuka Yesu Kristo.

Pia, amewataka Watanzania inapotokea mtu ameomba msamaha wasimuone ni mdhaifu maana hiyo ndiyo aina ya watu wanaotakiwa kwenye Taifa kwa watu kutoona tabu kujitoa, kujishusha na kudhalilika ili Taifa lipone.

Amesema kupitia kwa Yesu, Wakristu wanafundishwa  msamaha na inatakiwa kujiuliza wanasameheana kwa kiasi gani endapo mtu mwengine akimkosea mwenzie wanabaki nalo kwa muda gani.

“Tunakatazwa kulaani na kuapiza tunatakiwa tuwaombee adui zetu na hili ndilo ambalo kila Mkristu katika siku hii ya Pasaka anatakiwa kusema mchango wangu kwa Taifa langu ni kusamehe walionikosea, kwa sababu najua hiyo ni sadaka kubwa kuliko zote kwa baba wa mbinguni,” amesema Dk Nchimbi ambaye pia ni mgombea mwenza mteule wa urais.

Awali, Mwanzilishi wa Mtoko wa Pasaka na mwimbaji wa Injili, Christina Shusho amesema anamshukuru Mungu tamasha hilo kufikisha miaka mitatu kwa kuwa, haikuwa ni nguvu zake pekee bali kwa kushirikiana na mwimbaji mwenzie Rose Mhando.

“Kufikia hapa si nguvu zangu wala za Rose bali ni Mungu ametenda kwa ajili yetu na kushirikisha watu wengine na kutoa kibali cha kukubaliwa hadi kufanikiwa kupata mlezi wa Mtoko wa Pasaka ambaye ni mtumishi wa Serikali kaka yangu Masanja Kadogosa,” amesema Shusho.

Amesema walimchagua Mkurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Kadogosa ambaye alikubaliana nao kwa madai kuwa kilichotokea kuwa mlezi ni mipango ya Mungu na si vinginevyo.

Naye, Kadogosa amesema kuombwa kuwa mlezi anaamini si kwa jicho la Christina bali ni Mungu ndiye ameonesha njia ya wao kumchagua yeye.

“Wapo watu wengi mno wanaoweza kuwa walezi wa Mtoko wa Pasaka lakini nikashangaa kwanini mimi, naamini kuwa ni Mungu ana makusudi yake kwenye hili ndiyo maana wakanichagua,” amesema Kadogosa.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amesema uwepo wa uongozi imara ni sababu ya utawala wa amani ndani ya nchi.

“Ukiangalia katika ukumbi huu vijana wamejitokeza kwa wingi, hii yote ni kwa sababu ya amani iliyopo baada ya kuchaguliwa viongozi imara,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *