Dk Nchimbi ateta na mabalozi wa nchi nne

Dar es Salaam. Mabalozi wa nchi nne wanaowakilisha nchi zao Tanzania, wamejadili mambo manne na Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emanuel Nchimbi ikiwamo umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi.

Viongozi hao ni kutoka nchini za Marekani, Algeria, Uganda na India na waliofanya mazungumzo na katibu mkuu huyo wa CCM kwa nyakati tofauti leo Jumatano, Februari, 12 2025, katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba, jijini Dar es Salaam.

Balozi wa Algeria nchini Tanzania, Ahmed Djellal, amesema uhusiano wa kihistoria kati ya Tanzania na Algeria upoa zaidi katika harakati za ukombozi wa Afrika.

Balozi Djellal amesisitiza pia umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi baina ya nchi hizo kupitia sekta mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kubadilishana uzoefu wa kiuongozi na fursa za masomo.

Naye Balozi wa India nchini Tanzania, Bishwadip Dey amesema uhusiano kati ya Tanzania na India umeendelea kuimarika siku hadi siku.

“Ukitazama kwa undani, uhusiano huu unanufaisha pande zote mbili katika sekta za biashara, uwekezaji, teknolojia na afya,” amesema balozi huyo.

Naye Naibu Balozi wa Marekani Tanzania, Andrew Lentz amesisitizia umuhimu wa kuendeleza uhusiano wa muda mrefu baina ya nchi hizi mbili.

Akitoa salamu za serikali ya Uganda kwa Tanzania, Balozi wa Uganda nchini Tanzania, Kanali mstaafu Fred Mwesigye amesema chama tawala cha NRM na serikali inatambua na kuheshimu mchango wa Tanzania katika harakati za ukombozi barani Afrika.

Na amemuhakikishia Balozi Nchimbi kuwa uhusiano wa kidugu kati ya Tanzania na Uganda utaendelea kuimarika kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.

“Urafiki wa kihistoria kati ya Tanzania na Uganda umejengwa juu ya misingi imara ya mshikamano wa kikanda, ushirikiano wa kisiasa na maendeleo ya kiuchumi ambao utaendelea kuimarika kwa ustawi wa mataifa yetu,” amesema.

Viongozi hao pia wamempongza Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi kwa kupitishwa kuwa wagombea wa nafasi ya urais na Dk Nchimbi katika nafasi ya makamu wa rais kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.