
Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amemteua Said Kiondo Athumani kuwa Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA).
Kabla ya uteuzi huo, Athumani alikuwa Mkufunzi Mkuu Chuo cha Kodi cha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na mkurugenzi wa mawasiliano ya Rais Ikulu, Charles Hilary, ikiwa imesainiwa na Katibu Mkuu Kiongozi Zanzibar, Zena Said imesema uteuzi huo unaanza leo Februari 8, 2025.
Athumani anachukua nafasi ya aliyekuwa Kamishna Mkuu, Yusuph Mwenda ambaye aliteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Kamishna Mkuu wa TRA, Julai mosi, 2024 akichukua nafasi ya Alphayo Kidata aliyeteuliwa kuwa mshauri wa Rais kuhusu masuala ya kodi.
Tangu aondoke Mwenda, mamlaka hiyo ambayo imekuwa ikifanya vizuri katika makusanyo ikikaimiwa na Said Ali Mohamed.
ZRA imekuwa ikifanya vizuri katika makusanyo ya kila mwezi. Taarifa ya mamlaka hiyo ya Januari mwaka huu inaonyesha mamlaka ilikusanya Sh81.512 bilioni kati ya lengo la kukusanya Sh80.984 bilioni sawa na ufanisi wa asilimia 100.65.