Dk Mwinyi apongeza ushirikiano taasisi za dini serikalini

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema taasisi na madhehebu ya dini nchini yanawajibika kuisaidia Serikali kudumisha amani na kuhubiri upendo kwa masilahi ya jamii na Taifa.

Rais Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Februari 3, 2025 wakati akizungumza na Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Alex Malasusa na ujumbe wake uliofika Ikulu Vuga kumsalimia.

Taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Mkurugenzi wa Mawasilino ya Rais Ikulu, Charles Hilary, inaeleza kuwa, Dk Mwinyi amesema Serikali iko tayari kushirikiana na madhehebu ya imani zote kuhubiri amani, kudumisha upendo na umoja ndani ya jamii kwa kuwa ndio msingi wa maendeleo katika kila nyanja.

“Taasisi za dini zimekuwa na mchango mkubwa wa maendeleo ya jamii, hivyo ni vyema kwa viongozi na waumini  kuwa mstari wa mbele kuhubiri amani ili Serikali ifanye jukumu la kuleta maendeleo kwa ufanisi,” amesema.

Kiongozi huyo wa nchi ameeleza kufarijika na mchango unaotolewa na KKKT kwa jamii hususani katika masuala ya afya, elimu, maji na malezi ya yatima.

Hata hivyo, Dk Mwinyi ameushauri uongozi wa kanisa hilo kuwekeza katika sekta ya utalii, elimu, biashara na uwekezaji akisema  Serikali ipo tayari kushirikiana nao na kutoa kila msaada kufanikisha azma hiyo.

Amewahakikishia kwamba, Zanzibar sasa ina mazingira ya kweli ya kuleta maendeleo kwa kuwa na amani, umoja na upendo miongoni mwa wananchi jambo lililokosekana kwa muda mrefu.

Mkuu wa kanisa hilo, Askofu Malasusa ambaye pia ni Askofu wa Dayosisi ya Masahariki na Pwani, ameshukuru ushirikiano uliopo baina ya Serikali na kanisa hilo.

Amesema hatua hiyo ni kichocheo cha  mambo yote ya maendeleo yanayaofanywa na  kanisa pamoja na  kupongeza hatua za maendeleo katika ujenzi wa miundombinu, ubunifu na utekelezaji wa Sera ya Uchumi wa Buluu kwa mafanikio.