Dk Mpango avunja ukimya kuachia madaraka

Arusha. Makamu wa Rais Dk Philip Mpango amevunja ukimya na kueleza sababu za kuomba kupumzika nafasi hiyo ya ikiwa ni pamoja na kufanya kazi serikalini kwa muda mrefu na sasa anawaachia vijana wenye uwezo kubeba mzigo wa kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan.

Dk Mpango si wa kwanza kufikia uamuzi kama huo, mwaka 1990 aliyekuwa Rais wa Awamu ya Nne wa Zanzibar Sheikh Idris Abdul Wakil naye aliamua kutowania muhula wa pili Zanzibar baada ya kuongoza kuanzia Oktoba 24, 1985 hadi Oktoba 25, 1990.

Uamuzi wa Wakili ulitangazwa na mwenyekiti wa CCM Taifa, Mwalimu Nyerere wakati akitoa taarifa kwenye Mkutano Mkuu wa CCM kuhusu kuachia ngazi ya urais Zanzibar.

Wakili pia aliwahi kufananishwa na Jumuiya ya Vijana ya CCM na Rais wa Afrika Kusini, Nelson Mandela aliyekaa madarakani kwa awamu moja pekee, kuanzia mwaka 1994 hadi mwaka 1999.

Akizungumza leo Februari 11, 2025 jijini Arusha, Dk Mpango amesema amefanya uamuzi huo kwa dhati na kwamba kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 Watanzania wanakaribia milioni 64 na kati ya hao vijana ni asilimia 77, hivyo wapo wengi wanaoweza kubeba mzigo huo.

Amesema chaguo lililofanywa na CCM la kumteua Dk Emmanuel Nchimbi kuwa mgombea mwenza ni chaguo sahihi.

Dk Mpango alikuwa akizungumza kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan, kwenye kikao kazi cha tano cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) jijini Arusha.

“Simbachawene (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene) mchokozi, labda niseme kidogo, sensa ya watu na makazi 2022 wataalamu walioaidadavua wanasema asilimia 77 ya Watanzania sasa ni vijana,” amesema.

Akilifafanua hilo, Dk Mpango amesema ametumikia Serikali kwa muda wa kutosha na kuwa Julai mwaka huu anatimiza umri wa miaka 68.

“Chuo Kikuu peke yake nilifundisha miaka 14, Benki ya Dunia miaka mitano, sasa nikijumlisha miaka niliyokuwa msaidizi wa Kikwete (Rais Mstaafu wa awamu ya nne Jakaya Kikwete) Ikulu, Naibu Katibu Mkuu Hazina, Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango miaka sita, TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) mwezi mmoja, Waziri wa Fedha miaka mitano na miezi minne.

“Na sasa katika nafsi hii kubwa miaka mingine minne, jamani nadhani inatosha, bado nina nguvu. Yako mambo ambayo ninaamini kwamba ninahitaji nafasi kwa ajili ya kuchangia maendeleo ya taifa,” amesema na kuongeza kuwa;

“Moja kati ya vitu ambavyo vinanisumbua kwa utumishi huu ambao nimeueleza kwa kifupi, siyo Watanzania wengi wamepata bahati ya kutumika katika nafasi hizo nyeti kama mimi, ninafikiri ninao mchango wa kuwaachia Watanzania wenzangu fikra yangu juu ya maendeleo ya Taifa hili,” amesema.

Dk Mpango ametumia nafasi hiyo kuwaomba viongozi wengine pale inapowezekana kutumia muda kuandika ili waliachie taifa hilo kumbukumbu nzuri na historia kwa kuchangia historia nzuri ya Tanzania.

“Kwa hiyo ni uamuzi ambao nimefanya kwa dhati, Watanzania sasa tunakimbilia milioni 64 vijana wako wengi, nilipokuwa naangalia vijana wa Tehama ni vijana kweli na wanafanya mambo makubwa, ninaamini kwamba wapo Watanzania ambao ni vijana na wanaweza kubeba mzigo wa kumsaidia Rais kikamilifu bila wasiwasi wowote.

“Na mimi naamini chaguo lililofanywa na chama chetu ni chaguo sahihi, kwa hiyo ndugu yangu George, umesema mwenyewe ukipanda treni muhimu kujua unapandia kituo gani, muda gani na unateremka muda gani na kituo gani, la sivyo litakupitiliza, niliamua kwamba nadhani ni vizuri yale mengine ningependa kufanya katika kuchangia maendeleo ya nchi yetu katika nafasi tofauti,” amehitimisha.

Awali, Simbachawene aliomba kuzungumzia DK Mpango, hasa kufuatia tangazo la kuomba kupumzika nafasi hiyo katika Mkutano Mkuu wa CCM Dodoma, kwani walilipokea kwa mshangao.

“Tukiwa pale tukamsikia Rais akisema ulipoona unamweleza haikuwezekana ukaamua kuandika barua ya kwamba unaomba upumzike. Jambo hili siyo tu limetushangaza lakini pia limetupa fundisho kubwa Watanzania,” amesema na kuongeza;

“Uamuzi wako wa kupumzika na wengine wakasema mgonjwa, mgonjwa gani huyu anatembea, si tunamuona hapa, ni uamuzi wa kizalendo, unaoifundiha Tanzania na dunia  kwamba uongozi wa kisiasa kama ambavyo imezoeleka na hata humu kwetu, maana hata mimi siko tayari kuuacha ubunge.

“Bado kabisa naona kiti nakalia vizuri, lakini kwako wewe umeridhika na kusema nilivyochangia mchango wangu umetosha, ni kitu cha kipekee, umetufundisha wanasiasa wa Tanzania na dunia kwamba kama wengine wanavyotamani vitu viwili vinatamanisha kubaki navyo ni pesa na madaraka,” amesema.

Simbachawene amesema Dk Mpango amewafundisha kuwa vitu hivyo havimsumbui wala havimletei shida, ndiyo maana ameamua kusema anataka apumzike, hivyo amewaachia tafakuri kujitafakari waliokaa kidogo na wale wanaotafuta madaraka kwa nguvu, kudhani wanajifurahisha mioyo yao kwa kukaa kwenye madaraka.

‘”Kumbe kwako wewe furaha yako ni kupumzika, msafiri mzuri ni yule anayejua pa kupandia basi, lakini anajua pia na mahala pa kushukia, umetufundisha hilo, nichukue nafasi hii kukuponegza sana, nilikushangaa lakini nikapata cha kujifunza,” amesema.

Alichosema Rais Samia

Katika mkutano mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) uliofanyika Dodoma, wakati wa kuchagua mgombea mwenza, Rais Samia alisema Makamu wa Rais alikuwa amekwenda kumuona na kumuomba ampumzishe, hivyo ni lazima wateua mrithi wake.

“(Mpango) ana sababu kadhaa lakini siyo za mahusiano ya kazi. Ana miaka 68 na angependa kuishi zaidi ikiwezekana agonge 90 huko. Aliniambia mama yake aliyemzaa alifika 88 na angependa ampite mama yake kidogo asogee mbele.

“Sasa (akamwambia) hizi pilika mnazoniingiza sitafika huko. Naomba nipumzisheni. Nikambishia-bishia, wiki iliyopita hapa akanikabidhi barua yangu hii. Kama hunijibu kwa mdomo barua yangu hii na barua pia sikumjibu,” alisema.

“Tulipokwenda kuzungumza na kamati kuu nikaieleza hiyo hali na wajumbe wote tukakubaliana tumpumzishe. Lakini nataka niwaambie, mambo makubwa na mafanikio tuliyoyaona ni kwa sababu ya msaada mkubwa wa mbobezi wa uchumi.

“Tumefanya kazi kwa ushirikiano mkubwa sana. Nimemtuma sana na wala halalamiki. Kwenye kamati kuu tumekubaliana tumshukuru sana sana kwa kazi anayotufanyia na atakayoendelea kutufanyia mwaka mzima unaokuja lakini bado ana 68 ninaweza kumtumia,” alieleza Rais Samia katika mkutano huo uliofanyika Januari 19, 2025 na ambao ulimchagua Rais Samia kuwa mgombea urais uchaguzi mkuu 2025 na Balozi Nchimbi kuwa mgombea mwenza.