Dk Mpango ataka uwekezaji kuhamia nishati safi

Dar es Salaam. Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, amesema ni muhimu kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara kutumia fedha zinazokusanya kutoka nishati zinazotumika sasa kuwekeza katika nishati safi.

Amesema kwa kufanya hivyo, mataifa hayo yatafanikiwa kuendana na mageuzi ya nishati kutoka chafu kwenda safi, ambao ndiyo mwelekeo wa dunia kwa sasa.

Kauli ya Dk Mpango inaendana na mkakati wa Serikali wa kuhakikisha inahamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Katika mkakati wa nishati safi ya kupikia, Tanzania imelenga kufikia mwaka 2034 angalau asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati hiyo.

Dk Mpango amesema hayo leo Jumatano Machi 5, 2025 alipofungua mkutano wa 11 wa mafuta na gesi Afrika Mashariki, unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.

Amesema kwa sehemu kubwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara bado zinaendelea kutumia nishati zisizokubalika kama vile makaa ya mawe na mafuta.

Ili kuendana na mwelekeo wa dunia, amesema wakati nishati hizo zinatumika, fedha zinazopatikana zinapaswa kuwekezwa kwenye miradi ya nishati safi.

“Tukiwekeza fedha tunazopata kwenye nishati zilizopo sasa, kuanza uwekezaji wa miradi ya nishati safi, tutafanikiwa haraka kuendana na mabadiliko ya nishati,” amesema.

Kwa sababu changamoto iliyopo kwa mataifa hayo ni rasilimali fedha, amesema mbinu hiyo ni wezeshi katika kuhamia matumizi ya nishati safi.

Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Philip Mpango akifurahia jambo na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko nje ya Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam mara baada ya kufungua Mkutano wa 11 wa Petroli wa Afrika Mashariki.

Hata hivyo, amesema kwa sasa Tanzania ni kinara wa nishati safi hasa katika eneo la kupikia na imeweka mikakati mbalimbali ya kufanikisha hilo.

Dk Mpango pia amezungumzia umuhimu wa matumizi ya teknolojia za kisiasa katika kuiendea nishati safi.

Ametaka kuwe na uhakika kuwa, teknolojia zinazotumika kuhamia kwenye nishati safi hazizalishi nishati chafu.

Amesema sekta ya mafuta na gesi zimekuwa na mchango chanya katika mchanganyiko wa nishati na maendeleo ya teknolojia yamewezesha kuwepo mbinu mpya za kuzidua.

“Kwa faida ya kizazi cha baadaye, sera na sheria zinapaswa kuweka wazi kwamba fedha zinazopatikana katika nishati zinazotumika ziwekezwe kwenye nishati safi,” amesema.

Ametaka mataifa ya Afrika kuendeleza mikakati ya kuchochea nishati mchanganyiko. Amesema ubia wa sekta ya umma na binafsi upewe nafasi kufanikisha hilo.

Amesema kuna umuhimu wa mataifa kushirikiana katika mageuzi ya nishati kutoka chafu kwenda safi.

Dk Mpango amesema elimu iendelee kutolewa ili kuwe na uelewa wa pamoja na kila mtu aone umuhimu wa mageuzi.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko, amesema kadri uchumi unavyokua, ndivyo mahitaji ya nishati yanavyoongezeka.

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo pamoja na viongozi wengine wa serikali wakiwasili katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam leo Jumatano Machi 5, 2025.

 Amesema kwa kulitambua hilo, Serikali ya Tanzania imekuwa ikifanya uwekezaji kuhakikisha inaongeza upatikanaji wa nishati.

Amezungumzia uwekezaji unaofanywa na Serikali hasa katika upatikanaji na nishati ya gesi asilia. Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Mafuta wa Kenya, Opiyo Wandayi, amesema nchi hiyo imefanya tafiti mbalimbali za kisayansi kuonyesha wawekezaji maeneo ya kuwekeza katika nishati.

Amesema Taifa hilo limewekeza katika miundombinu na miradi kuwezesha kuifikia rasilimali nishati.

Ametaka nchi za ukanda wa Afrika Mashariki zishirikiane kufanya kazi pamoja kufikia fursa za nishati zilizopo.

Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini wa Uganda, Dk Ruth Ssentamu, amesema miundombinu ya umeme inahitaji uwekezaji wa fedha.

Amesema wameona juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania akiwa kinara wa nishati safi ya kupikia.

Ameeleza furaha yake kutokana na kuanza kwa utekelezwaji wa mradi wa Bomba la Mafuta kutoka Hoima hadi Tanga, Tanzania.

Amesema hatua hiyo ni uthibitisho wa juhudi za kikanda katika kuhakikisha kunapatikana nishati ya uhakika.

Dk Ruth amesema kwa pamoja itawezekana kutumia rasilimali zilizopo. “Kama tutakwenda pamoja, tutaona matokeo ya mageuzi halisia,” amesema.