Dk Mpango ahimiza benki kutumia akili mnemba

Arusha. Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amezihimiza taasisi za kifedha nchini kukumbatia matumizi ya teknolojia ya akili mnemba (AI), huku akisisitiza umuhimu wa kuongeza ulinzi wa mtandao.

Pia, amezitaka taasisi hizo kuwekeza katika teknolojia za kisasa ili kupunguza gharama za uendeshaji, kuongeza ushirikishwaji na kuboresha uzoefu wa wateja.

Akizungumza leo Ijumaa Mei 16, 2025 alipofungua semina ya wanahisa wa Benki ya CRDB jijini Arusha kabla ya Mkutano Mkuu wa Mwaka (AGM) wa benki hiyo unaotarajiwa kufanyika Mei 17, Dk Mpango amesema matumizi ya AI katika sekta ya benki yanaweza kuchochea mabadiliko makubwa na kufikia wakazi wengi wa vijijini na walio nje ya mfumo wa kifedha.

“Uwekezaji katika teknolojia, hasa AI, hautaongeza tu ufanisi na tija na kupunguza gharama, bali pia utaleta huduma za kibenki karibu na watu,” amesema.

Ametaka benki kuona AI kama chombo muhimu cha kulinda mitaji yao na kukuza idadi ya wateja.

Dk Mpango ameonya kwamba, kuongezeka kwa matumizi ya teknolojia kunakuja na ongezeko la hatari za usalama wa mtandao, hivyo ameagiza taasisi za fedha kuimarisha miundombinu yao ya kidijitali kujikinga na uhalifu wa mtandao, uvujaji wa data na udanganyifu.

“Teknolojia lazima iendane na usalama wa mtandao. Hatima ya kibenki inategemea jinsi tunavyooanisha ubunifu na ulinzi wa mtandao,” amesema.

Amekariri utafiti wa Shirika la Ushirikiano na Maendeleo la Uchumi (OECD) uliochapishwa Februari, 2025 akisema zaidi ya Dola za Marekani trilioni 10 zinatarajiwa kuwekezwa duniani miaka 10 ijayo kuimarisha mapambano dhidi ya uhalifu wa mtandao.

Amesema AI na roboti zinatarajiwa kuchukua jukumu kubwa katika kazi za kibenki na bima, hivyo amesisitiza ni muhimu benki za Tanzania kuendeleza mabadiliko ya kiteknolojia.

Dk Mpango ametaka benki kuchunguza uwezekano wa kupokea mali za kidijitali na teknolojia za blockchain, akishauri taasisi za fedha kuanza kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Chama cha Benki Tanzania (TBA) kuandaa mfumo wa kisheria utakaoruhusu kuingia kwa usalama na kwa udhibiti katika sekta ya mali za kidijitali.

Akizungumzia maendeleo ya sekta ya fedha katika miongo mitatu iliyopita, ametaja mageuzi ya kifedha ya miaka ya 1990 yaliyowezesha kuibuka benki za kibiashara kama ya CRDB.

Mageuzi hayo amesema yalikuwa na mchango mkubwa katika kuboresha ushindani, ufanisi na udhibiti wa kifedha.

Maendeleo mengine ya sera, ikiwamo Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha (BFIA) na mifumo ya ushirikishwaji wa kifedha na elimu, amesema yamechochea ujenzi wa mfumo wa kifedha imara.

Benki ya CRDB ilitambuliwa kwa mchango wake katika uvumbuzi wa kidijitali na ushirikishwaji wa kifedha kupitia bidhaa kama SimBanking na CRDB Wakala zilizoiwezesha kupanua huduma hadi maeneo ya vijijini ambako matawi ya kibenki ya kawaida hayajafunguliwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema mabadiliko ya benki hiyo yametokana na uwekezaji katika teknolojia ya kidijitali na kuzingatia ubunifu unaolenga wateja.

Kuanzia matawi 19 mwaka 1996, CRDB sasa ina matawi zaidi ya 260 nchini na imeibua zaidi ya asilimia 95 ya suluhu za kibenki zinazotumika sokoni.

Miongoni mwa vumbuzi hizo ni TemboCard, ATM, huduma za PoS, benki za mtandao na simu, na hivi karibuni, CRDB Al Barakah inayohusiana na sharia za Kiislamu.

CRDB pia imeongoza katika sekta ya bima kwa kuzindua tawi la CRDB Insurance na kutoa hati fungani ya kwanza ya kijani ya Tanzania na hati fungani ya miundombinu ya barabara (Samia Infrastructure Bond).

Benki hiyo imepanua shughuli zake nje ya mipaka ya Tanzania, kwa kuanzisha CRDB Bank Burundi mwaka 2012 na kuingia katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) mwaka 2023.

CRDB ni benki kubwa zaidi nchini kwa miongozo ya mali, ikiwa na mali ya Sh16.6 trilioni mwaka 2024.

Inaongoza kwa amana (Sh10.9 trilioni) na mikopo (Sh10.4 trilioni) na ilipata faida ya Sh551 bilioni baada ya kodi mwaka jana, mabadiliko makubwa kutoka kwenye hasara zilizopatikana mwaka 1996.

Benki hiyo bado ni miongoni mwa walipakodi wakubwa nchini na inaendelea kutoa faida nzuri kwa wanahisa wake, ikiwamo Serikali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *