Dk Mpango: Afrika iimarishe umoja kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi

Unguja. Nchi za Afrika zimesisitizwa kuimarisha umoja ili kusukuma mbele ajenda ya pamoja katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

Pamoja na kuimarisha uwezo wa kutafuta rasilimali za ndani, pia zimetakiwa kuacha kutegemea ufadhili kutoka mataifa makubwa, huku zikiendelea kuathiriwa na athari za mabadiliko hayo.

Hayo yameelezwa leo Jumatatu Aprili 28, 2025 katika mkutano wa Kundi la Wataalamu wa Majadiliano ya Mabadiliko ya Tabianchi Afrika (AGN), unaoendelea kisiwani Zanzibar na kuwahusisha wadau wa mazingira kutoka mataifa 54 ya Afrika.

Akifungua mkutano huo wa siku tatu, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango kupitia hotuba iliyosomwa kwa niaba na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema Afrika bado inaathiriwa kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya tabianchi, hivyo ni muhimu kwa nchi za Afrika kupaza sauti kwa pamoja.

“Athari za mabadiliko ya tabianchi zinaendelea kuongezeka huku kukiwa na upungufu mkubwa wa fedha za kukabiliana na changamoto hizi. Mkutano huu ujadili na kutoa sauti ya pamoja, tukitanguliza vipaumbele vyetu kama bara,” amesema Dk Mpango.

Pia, amesema ingawa Afrika inachangia kwa kiwango kidogo kuharibu mazingira, bado inapokea kiasi kidogo cha fedha za kushughulikia athari hizo.

Hivyo, amezihimiza nchi wanachama kujikita katika kutafuta fedha za ndani, badala ya kutegemea misaada kutoka mataifa tajiri, kwa kuwa upatikanaji wa fedha unazidi kupungua.

“Fedha zinapatikana kwa shida kutokana na changamoto za kisiasa duniani na nchi za Afrika zimebeba mzigo mkubwa wa madeni. Tunapaswa kushinikiza mataifa yaliyoendelea kupunguza au kusamehe madeni yetu,” amesema makamu huyo wa Rais.

Pia, Dk Mpango amesisitiza umuhimu wa kuwekeza katika nishati safi na madini ili kuongeza mapato akisema Afrika imesalia nyuma katika biashara ya hewa ukaa na kunufaika kidogo huku akitaka mjadala wa mkutano huo utafute majibu kwa changamoto hiyo.

Amesema Afrika inahitaji zaidi ya Dola 300 milioni za Marekani kila mwaka ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Mwenyekiti wa AGN, Dk Richard Muyungi amesema katika kujadili nishati za mpito, Bara la Afrika bado lina zaidi ya watu milioni 900 wasio na nishati safi ya kupikia na zaidi ya milioni 600 hawana nishati ya kawaida.

“Bado kuna watu hawajui jinsi ya kupika kwa kutumia nishati safi na wengine hawajaunganishwa na umeme. Hatuwezi kuzungumzia nishati za mpito bila kushughulikia changamoto hizi za msingi,” amesema Dk Muyungi.

Amesema mkutano huo pia utajadili namna Afrika inavyoweza kunufaika na fursa za dunia katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, hasa kwa kutumia nguvu kazi ya vijana wa Afrika katika sekta ya nishati mpya.

Dk Muyungi  amesema biashara ya hewa ukaa bado haieleweki vizuri kwa wananchi, ingawa ni sekta muhimu inayochangia uchumi wa dunia, lakini bado haijalinufaisha Bara la Afrika kutokana na changamoto za bei na uelewa mdogo.

Mwakilishi wa UNEP, Clara Makenya amesema Afrika inapaswa kuzungumza kwa sauti moja na kuhakikisha vipaumbele vyake vinaakisiwa katika mipango na programu mbalimbali, hasa katika sekta ya kilimo.

Mwakilishi wa G20, Maesela Kaekena amesema vipaumbele vimewekwa kushughulikia masuala kama uhifadhi wa bahari, ardhi na kupambana na mmomonyoko wa udongo, huku akisisitiza uchafuzi wa mazingira hasa unaotokana na plastiki, bado ni changamoto kwa nchi za Afrika.

Naibu Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Lise Abildgaard Sorensen, amesema licha ya Bara la Afrika kuchangia kidogo katika mabadiliko ya tabianchi inaathirika zaidi.

Amesema nchi za Bara la Ulaya ziko tayari kuisaidia Afrika kukabiliana na changamoto hizo.

“Afrika mnapaswa kuwa na umoja, tunataka kuona Afrika ikishirikiana kikamilifu katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Hili sio suala la hiari bali ni wajibu,” amesema balozi huyo.

Mkurugenzi wa Uhimilivu wa Mazingira na Uchumi wa Buluu wa Umoja wa Afrika, Harsen Nyambe amesema Afrika iko njia panda na inapaswa kujikomboa yenyewe kwa kuweka msingi imara wa kushughulikia changamoto hizo.

“Hatupaswi kuendelea kutegemea ahadi zisizotekelezwa. Fedha za kukabiliana na changamoto hizi zinapaswa kupatikana na kutumika ipasavyo kusaidia maendeleo ya bara letu,” amesema Nyambe.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *