Dk Manguruwe afikisha siku 141 gerezani, upelelezi haujakamilika

Dar es Salaam.  Mkurugenzi wa kampuni ya Vanilla International Ltd, Simon Mkondya (40), maarufu Dk Manguruwe, anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi, anaendelea kusota rumande kwa siku 141 sasa kutokana na upelelezi wa kesi hiyo kutokamilika.

Mkondya na mwenzake, mkaguzi wa fedha wa kampuni hiyo, Rweyemamu John (59), ambaye yupo nje kwa dhamana, wanakabiliwa na mashitaka 28 yakiwemo ya kuendesha biashara ya upatu na utakatishaji fedha linalomkabili Mkondya peke yake.

Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao wamefikishwa mahakamani hapo Novemba 5, 2024 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi ya mwaka 2024.

Hata hivyo, tangu siku hiyo hadi leo Machi 26, 2025, Mkondya amefikisha siku 141, ambazo ni sawa na miezi minne na siku 21, akiwa rumande kutokana na mashitaka ya kutakatisha fedha yanayomkabili kutokuwa na dhamana.

John ambaye ni mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo, yupo nje kwa dhamana baada ya kwenda kuomba dhamana Mahakama Kuu na pia hana mashitaka ya kutakatisha fedha.

Leo, Wakili wa Serikali, Winiwa Kasala ameieleza Mahakama hiyo, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Anna Magutu kuwa Serikali bado inaendelea na uchunguzi, hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hata hivyo, mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, Mkondya hakuletwa mahakamani hapo kutoka gerezani, lakini mshtakiwa wa pili ambaye yupo nje kwa dhamana alikuwepo mahakamani hapo.

Hakimu Magutu alikubaliana na upande wa mashitaka na kuahirisha kesi hiyo hadi Aprili 8, 2025.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, kati ya mashitaka hayo 28,  19 ni ya kuendesha biashara ya upatu na tisa ni ya kutakatisha viwanja.

Katika shitaka la kuendesha upatu, washtakiwa wanadaiwa kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba Mosi, 2023, jijini Dar es Salaam, walitenda makosa hayo

Inadaiwa kuwa Mkondya akiwa kama mkurugenzi wa kampuni hiyo na John akiwa mkaguzi wake waliendesha biashara ya upatu kwa kuwaahidi watu watapata pesa mara mbili hadi tatu kama faida zaidi ya waliyotoa.

Washtakiwa hao wanadaiwa kujipatia Sh92.2 milioni kutoka kwa watu 19 tofauti ambao walitoa kiasi tofauti cha fedha kwa kuwaahidi kuwa watapata faida mara mbili hadi tatu ya fedha walizotoa.

Katika mashitaka tisa ambayo ni ya utakatishaji fedha yanayomkabili Mkondya pekee yake, inadaiwa kuwa kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba Mosi, 2023 akiwa katika Mkoa wa Dar es Salaam na akiwa kama mkurugenzi wa kampuni hiyo, alijipatia jumla ya viwanja tisa vilivyopo katika kitalu namba AB eneo la Idunda mkoani Njombe.

Pia, Mkondya anadaiwa kujipatia viwanja hivyo huku akijua viwanja hivyo ni mazalia ya makosa tangulizi ya kuendesha biashara ya upatu.

Kwa mara ya kwanza washtakiwa hao wamefikishwa mahakamani hapo Novemba 5, 2024 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi ya mwaka 2024.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *