Dk Biteko: Tuondoe mifumo kandamizi kazini inayoumiza wanawake

Dar es Salaam. Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko ametaka kuwapo  kwa mazingira salama na wezeshi kwa wanawake kazini,  kuondoa ubaguzi wa kijinsia na mifumo kandamizi ambayo itawafanya wajione kuwa duni mahali pa kazi.

Amesema ni vyema kuangalia hali zao za kibaiolojia na kutozitumia kama kikwazo kwao kushiriki katika uchumi wa madini.

Ametoa kauli hiyo katika hafla ya usiku ya Pre-IWD (hafla kabla ya kufikia siku ya kimataifa ya wanawake duniani) ambayo iliwakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya madini, kujadili ushiriki wa wanawake katika mnyororo mzima wa thamani ikiratibiwa na Azurite Management & Consultancy na EcoGraf.

Dk Biteko amesema Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kuhakikisha wanawake wanakuwapo katika shughuli zote za kiuchumi nchini, hivyo ni lazima mazingira wezeshi yatengenezwe na si kandamizi.

“Sisi kama wasaidizi wake tutaendelea kuhakikisha kuwa alipo mwanamke anapata haki sawa na mwanaume, mwamke habaguliwi, havutwi shati wala kurudishwa nyuma kwa sababu ya jinsia yake kufanya hivi ni makosa,” amesema Dk Biteko.

Amesema mwanamke anatakiwa apewe nafasi sawa na mwanaume kwa sababu wamethibitisha kuwa wanaweza na wakati mwingine zaidi ya wanaume.

“Mwanaume na mwanamke, nafasi ya mwanamke kutokuwa mwaminifu ni ndogo sana kuliko mwanaume, Serikali itaendelea kuwapa kipaumbele wakati wote ili mjisikie kuwa ni jumuiya ya Watanzania na hamuhitaji kubebwa maana mnajibeba wenyewe katika nyanja zote za kiuchumi.”

Amesema kinachofanyika sasa ni kuhakikisha mtoto wa kike anapata heshima sawa na mwanaume, anasoma na kufundishwa kama mtoto wa kiume na akiomba kazi apangiwe.

“Hili lifanyike huku ukijua kuwa ana uwezo wa  kufanya kazi na isichukuliwe kama amesaidiwa kwa sababu ni mwanamke,” amesema Dk Biteko.

Amesema jambo lolote linapofanywa kwa nia ya kumsaidia mwanamke itakuwa ni kutweza na kumuona kama hawezi wakati anaweza kufanya kazi sawa na mwanaume.

“Hivyo niwatake wadau mbalimbali, kuwapa kipaumbele wanawake kushiriki katika shughuli za kiuchumi, kuwapa fursa za kielimu na kumiliki rasilimali, kushiriki katika majadiliano na vikao mbalimbali vya kufanya maamuzi kwenye sekta hiyo,” amesema.

Hiyo ni kwa sababu, ripoti ya Benki ya Dunia (WB) ya mwaka 2024 inaonyesha kuwa wanawake wanaojishughulisha katika uchimbaji mdogo wa madini ni moja ya tatu ya watu wote waliopo katika sekta hiyo, huku akisisitiza kuwa ni muhimu kuhakikisha wanawake wanaongezeka.

Waziri wa Madini, Antony Mavunde amesema Serikali inaamini kupitia sera na sheria zilizowekwa itamsaidia mwanamke aweze kushiriki ipasavyo katika mnyororo wa thamani.

Mwandaaji na Mkurugenzi wa Azurite Management & Consultancy, Christer Mhingo amesema mbali na kuwapo kwa makongamano kama hayo pia wamekuwa wakiwajengea uwezo wanawake waliopo katika sekta ya madini, nishati kupitia programu zinazofanyika mikoa mbalimbali nchini.

“Maeneo ambayo tumeyafikia ni pamoja na Ulanga- Morogoro, Tanga, Arusha pia tumefanya programu hizi kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari,” amesema.