Dar es Salaam. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amekemea matumizi ya lugha za kumdhalilisha mwanamke kwa sababu ya jinsia yake, katika kampeni za uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.
Ametoa rai hiyo akiwahamasisha wanawake kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi huo, badala ya kuwa wapigakura pekee.
Dk Biteko ametoa rai hiyo katika jukwaa la The Citizen Rising Woman awamu ya tano linalofanyika leo Machi 7, 2025 katika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam lililoandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kwa ushirikiano na Crown Media na wadau mbalimbali.
Amesema kuwapo kwa lugha za udhalilishaji kunawafanya wanawake kuwa na kazi nyingi za kufanya wakati wa kugombea.
“Hali hii inamfanya awe anapambana kunadi sera na ana changamoto ya kupambana na mfumo uliomdunisha, anakuwa na vita mbili kwa wakati mmoja wakati ambao mwanaume una vita ya kutaka kura pekee, huku mwanamke anatakiwa kuuaminisha umma kuwa anaweza kuwa sawa na mwanaume,” amesema.
Amesema ikiwa hicho hakitabadilika kizazi kijacho cha mabinti kitaamini kuwa nafasi za uongozi ni za wanaume.
“Niwatake wanawake muende mkapambane muende kushinda uchaguzi kuelekea malengo mliyonayo,” amesema.
Dk Biteko ameipongeza MCL kwa kuja na jukwaa hilo kwa kuwa limeleta mafanikio.
“Niwapongeze Kampuni ya Mwananchi kwa mpango mzuri wa The Citizen Rising Women kwani kwa kipindi chote cha miaka mitano tangu kuanza kwake, tayari zimeandikwa makala zenye simulizi mbalimbali kwa kuwatangaza na kuwaorodhesha wanawake, kuendelea kujifunza na kuhamasisha kupitia simulizi zaidi ya 250,” amesema.
Amepongeza kitendo cha kuwakutanisha wanawake, taasisi na wadau mbalimbali bila kuwasahau wanaume Machi 8, kila mwaka ili kuzungumza masahibu yanayowakumba wanawake sehemu mbalimbali.
“Niwape pongezi taasisi zinazowapa wanawake nafasi za uongozi, naamini na MCL mtazidi kutoa nafasi zaidi kwa wanawake,” amesema.
Akizungumza kwenye kongamano hilo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi amewakumbusha Watanzania umuhimu wa kusoma kitabu kilichoandikwa na Mwalimu Julius Nyerere kuhusu wanawake.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi akizungumza leo Machi 7, 2025 wakati wa kongamano la jukwaa hilo linalofanyika Mlimani City, jijini Dar es Salaam lililoandaliwa na MCL kwa ushirikiano na Crown Media na wadau mbalimbali.
“Nyerere akiwa kijana wa miaka 22 na mwanafunzi wa mwaka wa pili aliandika kitabu kuhusu uhuru wa mwanamke, humo alimtaja mwanamke kama ndege tai kwamba anaweza kuruka juu zaidi na siyo kuku.
“Nikiangalia hii Rising Woman naona inaendana kabisa na kile alichoandika Mwalimu Nyerere kwamba, mwanamke anaweza kuruka juu na kuangazia dunia,” amesema.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema: “Sisi wananchi wa Mkoa wa Dar tunamthamini sana mwanamke, tuko bega kwa bega kuhakikisha yote wanayokusudia kuyafanya yanafanikiwa. Tutaendelea kuondoa mifumo yote kandamizi ili kuhakikisha tunakuwa sawa katika kila jambo.”

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila akizungumza leo Machi 7, 2025 wakati wa kongamano la jukwaa hilo linalofanyika Mlimani City, jijini Dar es Salaam lililoandaliwa na MCL kwa ushirikiano na Crown Media na wadau mbalimbali.