D’jaro Arungu mtangazaji mwenye dunia yake

Dar es Salaam. Jina la D’jaro Arungu si geni kwa wasikilizaji wengi wa redio nchini, mbali na umahiri wa kazi yake, mtangazaji huyo ana rekodi yake ya kipekee Bongo nayo ni ya kushinda tuzo 19 ndani ya miaka 10 kati ya 20 aliyodumu katika fani hiyo.

Safari yake rasmi ya utangazaji ilifuata mkondo sahihi mwaka 2004 ikiwa ni baada ya kuvutiwa na Godwin Gondwe ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Singida, na kuonyeshwa njia na Abdallah Mwaipaya ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Mtwara.  

Tangu wakati huo Arungu amefanya kazi na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) lakini kipindi chake cha Papaso kililichoanza kuruka hewani Januari 2015 kupitia TBC FM kisha TBC Taifa ndicho kimemfanya kuweka rekodi hiyo.

Kipindi hicho kinachocheza muziki, kufanya mahojiano na wasanii na kushirikisha wasikilizaji katika vipengele vyake vya moto, tangu mwaka 2015 kimemwezesha Arungu kushinda tuzo 19 za ndani na kimataifa akiwa mtangazaji pekee nchini mwenye rekodi hiyo.

Akizungumza na Mwananchi, D’jaro Arungu ameeleza kuhusu mafanikio ya kazi yake, jinsi safari ya utangazaji ulivyoanza na hatima yake katika tasnia hiyo katika kipindi hiki ambacho watangazaji maarufu wanatoka na kuingia katika redio mbalimbali.

Ikiwa ni takribani wiki moja tangu kushinda tuzo tatu kwa mpigo za E360 Awards 2025 zilizotolewa Nairobi, Kenya, Arungu anasema ushindi huo una maana kubwa kwake na haikuwe rahisi kama baadhi ya watu wanavyoweza kudhani.
Moja ya vipengele alivyoshinda katika E360 Awards 2025, ni Kipindi Bora cha Redio (Papaso) ikiwa ni tuzo ya pili kwa kipindi hicho kushinda, Arungu anasema hiyo inaonyesha ni kiasi gani watu wamekuwa  wakimfuatilia.

“Nimefurahi sana Papaso kushinda tuzo hii, inaonesha ni kwa kiasi gani watu wananifuatilia na kunipenda, kama wangekuwa hawafanyi hivyo isingeshinda maana hizi tuzo zinategemea kura kwa asilimia 100, hivyo ukiwa na kura nyingi unashinda,” alisema Arungu.  

Anasema Papaso ilianza mwaka 2014 kama kipengele ndani ya kipindi cha Swaga za Kikwetu lakini ilipofika 2015 ikabidi ndio ibebe jina la kipindi kizima maana aliona ni jina nzuri zaidi na jepesi watu kushika, na mwaka huo huo kikashinda Tuzo za Watu.

“Baada ya kufanya vipindi vingi, niligundua nimekuwa maarufu kuliko vipindi vyenyewe, sasa nikaumiza kichwa kipi nifanye, ndipo nikaja na hilo jina la Papaso na kweli watu wakaelewa, ukimtaja Arungu umeitaja Papaso, ukiitaja Papaso umemtaja Arungu,” alisema.  

Arungu amesema ni kweli kipindi chake kina wasikilizaji wengi vijijini kama ambavyo imekuwa ikidaiwa lakini haina maana kuwa hana wasikilizaji mjini, wa mjini wapo ndio hao kwa sehemu kubwa wanampigia kura mtandaoni hadi kushinda tuzo lukuki.

Tuzo 19 alizoshinda

Na hii ndio orodha ya tuzo za ndani na kimataifa alizoshinda D’jaro Arungu kati ya mwaka 2015 hadi 2025 ambapo anasema ushindi wake unatokana na kuwa karibu na wasikilizaji kwa kuwapa kila wanachohitaji, na pia kushirikiana na wengine.

Tuzo za Watu 2015 (Tanzania) – Mtangazaji wa Redio Anayependwa, na Kipindi Pendwa cha Redio (Papaso).  

Tanzania Instagram Awards 2016 (Tanzania) – Mtangazaji Bora wa Redio.

Bongo Music Awards 2023 (Tanzania) – Mtangazaji Bora wa Redio.

Ejat 2023 (Tanzania) – Makala ya Afya Redioni.

Zikomo Awards (Zambia)  2022 – Mtangazaji Bora wa Redio Afrika.

Zikomo Awards (Zambia)  2023 – Mtangazaji Bora wa Redio Afrika, na Mshawishi Bora Afrika.

Zikomo Awards (Zambia)  2024 – Mtangazaji Bora wa Redio Afrika.

MVAA Awards (Nigeria) 2024 – Mtangazaji Bora wa Redio Afrika, na Mafanikio ya Maisha Redioni.

Shining Star Africa Awards 2023 (Afrika Kusini) – Mtangazaji Bora wa Redio Afrika, na Mshawishi Bora Afrika.

Shining Star Africa Awards 2024 (Afrika Kusini) – Mtangazaji Bora wa Redio Afrika.

E360 Awards 2023 (Kenya) – Mtangazaji Bora wa Redio Afrika Mashariki.

E360 Awards 2024 (Kenya) – Mtangazaji Bora wa Redio Afrika Mashariki.

E360 Awards 2025 (Kenya) – Mtangazaji Bora wa Redio Afrika Mashariki, Kipindi Bora cha Redio (Papaso), na Mafanikio ya Maisha Redioni.

“Hakuna kikubwa ambacho kipo nyuma ya mafanikio yangu zaidi ya kufanya kazi kwa bidii, kushirikiana na wenzako na kumshirikisha msikilizaji,” anasema Arungu na kuongeza.

“Unajua mara nyingi baadhi ya watangazaji wakubwa na maarufu wanakuwa na tabia ya kuwavimbia wasikilizaji lakini hao ndio mabosi wetu na hao ndio wanatupigia kura, kwa hiyo mimi naishi nao vizuri,” anasema.

Alisema aina ya nyimbo anazocheza katika kipindi chake ni za kushirikisha wasikilizaji sio zile ambazo zimechezwa kuanzia asubuhi hadi jioni na hapo ndipo wasikilizaji wanapenda maana wanapata ladha tofauti.

“Mimi nachagua nyimbo ambazo hazijasikika sana ndio maana nimekuwa Baba Mzazi wa wasanii wengi, ninawatoa huko chini ambapo hata hawajulikani mpaka wanakuja kuwa mastaa wakubwa katika muziki wetu,” anasema Arungu.

Alisema aliposhinda Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (Ejat) 2023 kupitia makala yake ya afya redioni aliyoeleza mathara yanayoweza kumpata mtu anayetumia meno kama nyenzo ya kufungulia vinywaji kama soda, ushindi huo ulionyesha upande wake mwingine.

“Nilifurahi maana ilifikia hatua watu wanasema Arungu anashinda tuzo za kupigiwa kura lakini linapofikia suala la kutengeneneza kipindi kizuri kipelekwe huko kwa wataalam wakipime hawezi kutoboa lakini nikatoboa,” alisema Arungu.

Ilikuwaje hadi kujiunga TBC?

D’jaro Arungu anasema alikuwa anapenda utangazaji, kwa hiyo wale watangazaji aliokuwa anawakubali walikuwa marafiki zake, kwa muda wote alihakikisha anakuwa karibu nao ili wampe mbinu na njia za yeye kuwa mtangazaji bora.

“Kati ya marafiki zangu kipindi hicho alikuwa ni Godwin Gondwe, alikuwa ametoka Radio Free Africa akaja Times FM na baadaye akaenda Radio One, kwa hiyo wakati akiwa Times FM ndio nikamtafuta nikamueleza kiu yangu ya kuwa mtangazaji.

“Gondwe ndiye akaniunganisha na Abdallah Mwaipaya ambaye alikuwa bado TBC kabla ya kwenda radio One, basi Mwaipaya akaniambia pale TBC FM (wakati huo PRT) wanahitaji watangazaji hasa wa Kiingereza na mimi upande huo nipo vizuri, kwa hiyo nikaenda,” alisema.
 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *