Diwani wa CCM Kakonko auawa akitoka sokoni

Kakonko. Diwani wa CCM Kata ya Kiziguzigu, Mwalimu Martin Mpemba, amefariki dunia baada ya kudaiwa kupigwa kichwani na kitu chenye ncha kali.

Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia Aprili 3, 2025, katika Kijiji cha Ruyenzi, Kata ya Kiziguzigu, akiwa njiani kurejea nyumbani kutoka sokoni.

Mwalimu Mpemba, ambaye alikuwa akiwakilisha CCM katika kata hiyo, anadaiwa kushambuliwa na watu wasiojulikana, jambo lililosababisha majeraha kichwani na kufariki dunia akiwa njiani akipelekwa jijini Mwanza kwa matibabu zaidi.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma, Filemoni Makungu amethibitisha taarifa kuhusu kifo cha Mwalimu Mpemba, ambaye alifariki dunia saa 5:45 usiku.

Makungu amesema Mwalimu Mpemba amefariki dunia wakati akiwa njiani akipelekwa Hospitali ya Rufaa Bugando jijini Mwanza kwa matibabu zaidi.

Amesema kuwa kutokana na tukio hili, Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma linamshikilia mtu mmoja, ambaye jina lake halikuwekwa wazi, kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Makungu amesema kuwa upelelezi wa tukio hilo unaendelea na kwamba mtuhumiwa atafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.

Aidha, Makungu ameongeza kuwa Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi kuendelea kutii sheria na kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi.

Ameahidi kuwa Jeshi la Polisi litaendelea kuchukua hatua kali dhidi ya wale wote wanaojihusisha na vitendo vya kujichukulia sheria mkononi, ili kuhakikisha usalama na amani vinatawala katika jamii.

                                     

Katibu wa CCM Mkoa wa Kigoma, Christopher Palangyo, ameeleza kusikitishwa na tukio hilo na kusema kuwa chama kinashutumu vikali mauaji hayo.

Palangyo ametoa wito kwa Jeshi la Polisi kuhakikisha wahusika wa tukio hili wanakamatwa haraka na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Amesisitiza kuwa mauaji ya namna hiyo hayakubaliki katika jamii iliyostaarabika, na uchunguzi wa haraka ni muhimu ili kuondoa mashaka na wasiwasi uliosababishwa na tukio hilo miongoni mwa wananchi.

“Hili jambo halivumiliki,” alisema Palangyo, akiongeza kuwa, “hata kama kulikuwa na changamoto, ni bora kushughulikia masuala hayo kupitia vyombo vya kisheria, mkakutana na kuyamaliza, kuliko kujihusisha na vitendo vya kuviziana, hasa kipindi hiki tunapoelekea kwenye uchaguzi.”

Katibu huyo pia alisisitiza umuhimu wa amani na usalama katika kipindi hiki muhimu, na kutaka kila mtu atii sheria ili kudumisha utulivu katika jamii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *