
Katika hatua madhubuti za kukabiliana na changamoto za maji AMCOS walitoa wito wa kuendelea kushirikiana, kuhamasisha rasilimali ya maji na kuwa tayari kukabiliana na changamoto ili kuhakikisha utekelezaji wa maazimio na kufanikisha Dira na Sera ya Maji ya Afrika.
Devotha Kihwelo
Dar es Salaam. Mawaziri wa Maji ukanda wa Afrika Mashariki (AMCOW) wamekutana kwa ajili ya kupitisha taarifa ya sekretarieti kuhusu dira na sera ya maji kwa ukanda huo ambayo inawapa mwelekeo wa kukabiliana na changamoto ya maji katika kila Taifa.
Katika kikao hicho cha kimkakati, viongozi walipokea na kujadili ripoti ya kamati ya kiufundi ambayo ilikuwa inaangazia utafutaji wa wafadhili wapya, dira na sera, uamuzi wa wakuu wa nchi wa Afrika ya mwaka 2008 na kuwa na takwimu za maji chini ya ardhi.
Pia wamejadiliana kwa ajili ya kupeana mamlaka ya ufuatiliaji kwa wale wanachama wanaodaiwa ili baraza hilo liweze kujiendesha, huku Tanzania ikiwa inalipa ada yake kwa wakati.
Katika kupitisha hilo wanaangalia nchi wanachama wanapopitisha sera zao wafike nazo hadi ngazi ya chini, usalama wa maji, usafi wa mazingira, na maendeleo ya sekta hiyo barani Afrika, huku wakisisitiza umuhimu wa kuweka maji kama nguzo kuu ya maendeleo katika ajenda ya mwaka 2063 ya Umoja wa Afrika.
Akizungumza katika mkutano huo uliofanyika jijini Dar es Salaam leo Ijumaa Machi 7, 2025 Naibu Waziri wa Maji wa Tanzania, Kundo Methew kwa niaba ya Waziri Juma Aweso, amesema mkakati wa mkutano huo ni kuwa na takwimu za kutosha za kuwepo kwa maji ardhini.
Amesema Tanzania ina lita bilioni 126 za maji ikiwa bilioni 121 yapo juu ya ardhi huku bilioni tano yakiwa chini ya ardhi ambapo ni takwimu ya nchi hiyo pekee. Ndiyo maana wanahitaji mkakati wa kuwa na takwimu za kutosha za chini ya ardhi kwa ukanda wote wa Afrika Mashariki.
“Mkakati wa leo tunataka kuwe na takwimu za kutosha za maji yaliyopo chini ya ardhi maana yake tufanye uwekezaji wa kutosha ili tuweze kufanya utafiti, pamoja na mabadiliko ya tabianchi yanapokuja kutokea ni lazima kujua tunakuwa na mkakati gani wa kuyakabili mazingira ya aina hiyo,” amesema Kundo.
Amesema katika kukabiliana na mabadiliko hayo kwa Tanzania kumekuwa na miradi mbalimbali ikiwemo ya kutoa maji Ziwa Victoria.
Kundo amesema kikao hicho kilikuwa kinasisitiza sekretarieti kuhakikisha inafanya mazungumzo na wafadhili, huku wakiendelea kutafuta wengine wapya ili kuhakikisha taasisi hiyo inaendelea kujiimarisha kifedha na kuangalia njia ya kusaidia miradi kwa nchi wanachama iliyokumbwa na mabadiliko ya tabianchi.
Pia, amesema wamefanya uchambuzi kwa maazimio ya nyuma ambayo yamewapa matokeo chanya na yale yaliyofeli kutafutia majibu ya sababu ya kutofanikiwa kwake na kuyaingiza kwenye kipindi kijacho ili kufanyiwa kazi.
Naye, Makamu wa Rais aliyemaliza muda wake na Waziri wa Maji na Umwagiliaji nchini Kenya, Eric Mugaa amesema wanataka kuhakikisha kila Waafrika wana maji ya kutosha ya kunywa na ya umwagiliaji.
Amesema malengo yao ni kuhakikisha baraza hilo linajiweza kifedha na wanahitaji kila mwanachama analipa ada ya mwaka, ili waweze kutekeleza miradi na shughuli zake.
“Tupo na wafadhili wengi na tunaomba waendelee kutufadhili kwa sababu hatuna uwezo wa kujiendesha wenyewe na tumeongelea swala la maji yaliyo chini ya ardhi kama rasilimali kwa Afrika,” amesema Mugaa.
Viongozi hao walieleza kuridhishwa kwao na hatua zilizopigwa ndani ya kipindi cha miaka miwili, huku kanda ya Afrika Mashariki ikiendelea kudumisha msimamo wa pamoja katika masuala ya msingi yanayohusu maji na mazingira.
Aidha, walimkaribisha Makamu wa Rais mpya wa kanda hiyo ambaye ni Jumaa Aweso na kumtaka kuendeleza juhudi za kuhakikisha Afrika inapata maendeleo katika sekta ya maji, kwa kushirikiana na kanda nyingine za Umoja wa Afrika.
Mkutano huo umeibua matumaini mapya ya mageuzi katika sekta ya maji, huku washiriki wakikubaliana kuna haja ya kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi, ili kuhakikisha miradi ya maji inatekelezwa kwa ufanisi zaidi.
Mawaziri waliokutana wamesisitiza kuwa maji hayapaswi kuonekana tu kama rasilimali ya asili, bali kama nyenzo ya kiuchumi inayoweza kusaidia nchi za Afrika kupiga hatua katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Nchi zilizoshiriki katika mkutano huo ni Kenya, Rwanda, Ethiopia, Sudan Kusini, Uganda, Burundi, Comoro, Djibouti, Eritrea, Sudan, Somalia na Tanzania ambaye alikuwa mwenyeji.