Diplomasia: Ujerumani yafungua tena ubalozi wake nchini Syria

Ujerumani imefungua tena ubalozi wake nchini Syria, ambao ulikuwa umefungwa tangu mwaka 2012, duru za Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani zimeliambia shirika la habari la AFP wakati mkuu wa diplomasia ya Ujerumani akizuru nchi hiyo siku ya Alhamisi, Machi 20.

Imechapishwa:

Dakika 3

Matangazo ya kibiashara

Ujerumani imefungua tena ubalozi wake nchini Syria siku ya Alhamisi mbele ya waziri wake wa mambo ya nje ambaye amezitaka mamlaka za mpito kufanya kila linalowezekana kuhakikisha usalama nchini humo.

Miezi mitatu baada ya kuangushwa kwa Rais wa Syria Bashar Al Assad, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock amekabidhi rasmi funguo za ubalozi huo, uliofungwa mwaka 2012 kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Katika nchi hii iliyogawanyika kati ya jumuiya kadhaa za kidini, ambapo kipindi cha mpito kinasalia kuwa kigumu miezi mitatu baada ya kukimbia kwa Bashar Al Assad, Bi Baerbock anatarajiwa kufanya mazungumzo siku ya Alhamisi na Rais wa mpito wa Syria Ahmed Al-sharaa na Waziri wake wa Mambo ya Nje Assaad al-Shaibani.

Kulingana na vyanzo vilivyo karibu na Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani, “ubalozi huo una timu ndogo ya kisiasa na utaendelea kupanua uwepo wake, kulingana na hali.”

“Kutokana na hali ya usalama na uwezo mdogo wa nafasi,” masuala ya visa na stakabadhi za kibalozi zitaendelea kushughulikiwa kutoka Beirut, Lebanoni, vyanzo hivyo vimesema.

Kabla ya kufungwa kwake mnamo mwezi wa Januari 2012 na upunguzaji wa wafanyikazi uliofuata ambao ulifanyika kufuatia mzozo huo, ubalozi wa Ujerumani huko Damascus ulikuwa na wafanyakazi karibu hamsini.

Miongoni mwa nchi za EU, ubalozi wa Italia tayari umeanza shughuli zake huko Damascus. Ufaransa kwa sasa imerudisha bendera yake kwenye jengo lake na kumiliki majengo hayo, lakini bado hakuna shughuli za kibalozi ambazo zimeanza. Uhispania pia ilitangaza kuwa ilipandisha bendera yake juu ya ubalozi wake katikati mwa mwezi wa Januari.

“Mwanzo mpya”

Kabla tu ya kuondoka Lebanon kuelekea Syria, Bi Baerbock alitoa wito kwa mamlaka mpya kudhamini amani na usalama kwa Wasyria wote, wiki mbili baada ya mauaji magharibi mwa nchi hiyo ambayo yalisababisha vifo vya zaidi ya raia 1,500, wengi wao kutoka kwa wachache wa Alawite ambao ukoo wa Assad unatoka.

Ni ghasia mbaya zaidi tangu muungano unaoongozwa na kundi la Kiislamu la Sunni Hayat Tahrir al-Sham (HTS) kuingia madarakani.

Wasyria wengi “wanaogopa kwamba maisha katika Syria ijayo hayatakuwa salama kwa kila mtu,” Baerbock amesema katika taarifa.

Ameitaka serikali ya mpito ya Syria kuhakikisha inadhibiti “makundi ndani ya safu zake.”

Ameongeza kuwa serikali inapaswa kuwafungulia mashtaka wale waliohusika na ghasia hizo na kuhakikisha amani na ustawi kote nchini Syria, ambayo imekumbwa na miaka 14 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.

“Hii ni kazi kubwa inayoikabili serikali ya mpito ya Syria inayoongozwa na Ahmed Al-sharaa,” amesema.

Bi. Baerbock amesema atatumia safari yake kuiambia serikali ya Syria kwamba “mwanzo mpya” kati ya Ulaya na Ujerumani, kwa upande mmoja, na Syria, kwa upande mwingine, ni masharti ya Wasyria wote kufurahia uhuru na usalama, bila kujali imani zao, jinsia, au kabila.

Siku ya Jumatatu Ujerumani ilitangaza kwamba itachangia euro milioni 300 katika ujenzi mpya nchini Syria, kama sehemu ya mkutano wa wafadhili ulioleta pamoja ahadi za msaada wa euro bilioni 5.8.

Bi Baerbock alikuwa tayari ameitembelea Syria mnamo Januari 3 akiwa na mwenzake wa Ufaransa, Jean-Noël Barrot, ziara iliyoamrishwa na Umoja wa Ulaya.

Katika picha hii iliyotolewa na shirika la habari serikali y Syria, SANA, kiongozi mkuu wa Syria Ahmad Al-sharaa, ambaye zamani alijulikana kama Abu Mohammed al-Golani, kulia, anakutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock, kushoto, na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Noel Barrot, katikati, huko Damascus, Syria, Ijumaa, Januari 3, 2025 kupitia.
Katika picha hii iliyotolewa na shirika la habari serikali y Syria, SANA, kiongozi mkuu wa Syria Ahmad Al-sharaa, ambaye zamani alijulikana kama Abu Mohammed al-Golani, kulia, anakutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock, kushoto, na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Noel Barrot, katikati, huko Damascus, Syria, Ijumaa, Januari 3, 2025 kupitia. AP

Ziara hii ilikuwa imeenea kwenye mitandao ya kijamii baada ya Ahmed Al-sharaa kukataa kumpa mkono Bi. Baerbock. Kama ilivyo desturi kwa baadhi ya Waislamu wenye msimamo mkali, kiongozi huyo wa Kiislamu alimsalimia kwa kuweka mkono wake kifuani mwake, baada ya kushika vidole vya mwenzake wa Ufaransa Jean-Noël Barrot.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *